Dunia iko katika hali ya taharuki na sintofahamu:Guterres

23 Januari 2020

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema dunia hivi sasa iko katika hali ya taharuki na sintofahamu ikikabiliwa na mambo makubwa manne ambayo yanatishia mustakbali wa mamilioni ya watu na sayari yenyewe.

Guterres ameyasema hayo leo mjini Davos kwenye kongamano la kila mwaka la kimataifa la uchumi.  Akiyarejelea mambo hayo manne Guterres amesema vita vya mabadiliko ya tabianchi, utandawazi usio sawia, kuongezeka kwa mivutano ya kimataifa na pengo la kidijitali ni changamoto kubwa zinazohitaji suluhu ya haraka.

Mosi Vita vya mabadiliko ya tabianchi

Katibu Mkuu amesema binadamu wametangaza vita na maliasili na maliasili hiyo inapambana vikali. “tunahitaji kuvishinda vita hivi na ni lazima tuvishinde. Tutasambaratishwa na mabadiliko ya tabianchi na si sayari. Hii ni dhahiri kwetu kwamba tunahitaji kubadili mwelekeo, kwani athari za mabadiliko ya tabianchi ni mbaya kuanzia moto wa nyikani hadi ukame unaosababisha migogoro.”

Amesisitiza kwamba jumuiya ya wanasayansi imetueleza nini la kufanya. Lakini ukosefu wa utashi wa kisiasa haujaturuhusu kutimiza ahadi ya mkataba wa Paris.

Ameongeza kuwa ushiriki wa wachafuzi wakubwa wa mazingira ni muhimu katika vita hivi la sivyo tutakuwa tumekwisha, akihimiza kwamba uraibu wa makaa ya mawe Asia pia unapaswa kukoma.

Ametoa wito wa kuweka gharama ya juu kwa hewa ukaa, akitaka kubadili mwelekeo wa kodi kutoka kwenye kipato na kuwekwa kwenye hewa ukaa hali ambayo amesema itakuwa ni ushidi kwa kila upande.

Guterres amesema ana matumaini kwa kuona mabadiliko ya kwelekeo kwenye miji, maoni ya umma na vuguvugu la vijana. Pia anaamini kwamba bado dunia inaweza kuchagiza sekta za umma na binafsi kufanya mabadiliko ambayo ni ya lazima kwa kila mtu na sayari dunia.

Pili ongezeko la mivutano ya kimataifa

Amesema kuna mivutano ya kimataifa inayoendelea akitolea mfano ya kibiashara baina ya Marekani na Uchina na pia migawanyiko  kwenye Baraza la Usalama akisema hii inatishia hatari ya migawanyiko mikubwa duniani.

Tatu, utandawazi usio sawia

Watu wanashawishika kwamba utandawazi haufanyi kazi kwao, kushuka kwa imani katika taasisi za kisiasa.  Kama moja ya ripoti zetu ilivyodhihirisha jana, watu wawili kati ya watatu wanaishi katika nchi ambazo pengo la usawa limeongezeka. Usifanye makosa katika dunia ya sasa ongezeko la pengo la usawa linazamisha mashua zote.

Guterres amesema anashuhudia hamasa ya malengo ya maendceleo endelevu kila kona anayokwenda kuanzia kwa viongozi wa kisiasa katika ngazi ya kitaifa hadi mashinani, kwa wajasiriamali, wawekezaji, asasi za kiraia na wengine wengi.” Tunashuhudia hatua kubwa zinazopigwa kuanzia fursa za kupata huduma za afya ya uzazi hadi kwenye ongezeko la wanaoweza kutumia mtandao wa intaneti. Lakini tunachokishuhudia hakitoshi.”

Kwa sababu zote hizo tunazindua muongo wa utekelezaji wa maelengo ya maendeleo endelevu ifikapo 2030. Na kongamano la kwanza la hatua za SDG litakalofanyika Septemba litaainisha mchakato na kuweka mikakati ya mafanikio. Hivyo hebu na tuufanye mwaka 2020 kuwa muongo wa hatua na hebu tuufanye mwaka 2020 kuwa mwaka wa uharaka.

Natoa wito kwa nchi zote wanachama “wasikilizeni watu wenu, fungueni milango yote kwa wote kuweza kusikilizwa na tafuteni utangamano. Heshimuni uhuru wa kukusanyika kwa amani na kujieleza na lindeni maeneo ya umma na uhuru wa vyombo vya Habari.”

Nne Pengo na athari za kidijitali

Amefafanua kuhusu athari mbaya za ulimwengu wa dijitali akisema ziko  athari kwenye soko la ajira, kuenea kwa hotuba za chuki, Akili bandia AI hutoa uwezekano wa vitosho kama vile umiliki wa silaha hatari.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter