FAO yaungana na Japan kuimarisha ufuatiliaji wa misitu duniani
FAO yaungana na Japan kuimarisha ufuatiliaji wa misitu duniani
Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO litaimarisha uwezo wa mfumo wake wa ufuatiliaji wa misitu ulimwenguni na hii ni kutokana na ushirikiano wake mpya na shirika la anga za juu la Japan, JAXA.
Taarifa ya FAO iliyotolewa leo katika miji ya Tsukuba, Japan na Roma, Italia inasema kuwa makubaliano hayo ya miaka mitatu yatapanua wigo wa mfumo wa FAO wa kutathmini misitu na matumizi ya ardhi.
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FAO anayehusika na miradi, Daniel Gustafson amesema "kwa kuwa ukataji holela wa miti na kubadilika kwa matumizi ya ardhi vinaongoza katika utoaji wa hewa ya ukaa, taarifa za pamoja za setilaili zina dhima muhimu sana katika kusaidia nchi kufanikisha ahadi zao za mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi.”
Ni kwa mantiki hiyo, ubia huo utapanua wigo wa matumizi ya majukwaa ya FAO ya ufuatiliaji misitu na matumizi ya ardhi, majukwaa yatambuliwayo kama SEPAL na tathmini ya ufuatiliaji misitu, Global Forest Resources Assessment .
JAXA hutumia teknolojia ambayo ina mfumo wa kipekee wa kuwezesha kufuatiliaji matumizi ya ardhi duniani bila kujali wakati iwe ni usiku au mchana, iwe kuna mawingu au mvua na hukusanya taarifa kwenye maeneo yaliyo na uoto au la.
"Kwa zaidi ya miaka 20, JAXA imekusanya taarifa hizo ambazo ni muhimu kuelewa mabadiliko kwenye misitu na kutabiri mambo yajayo. Na JAXA inatarajia kuwa data zetu za setilaiti zinaweza kutumika kusaidia ufanyaji wa maamuzi,” amesema Imai Ryoichi, Makamu Rais wa shirika hilo la anga za juu la Japan akiongeza kuwa wako tayari kuchangia katika maeneo ya mbali zaidi.
Pamoja na kutoa data hizo, JAXA itaendesha mafunzo kwa nchi wanachama wa FAO.
Mfumo wa FAO wa kufuatilia misitu ukiwemo huo wa SEPAL , una zaidi ya watumiaji 4,300 kutoka nchi 160 na huwapatia uwezo wa kupata taarifa za kufuatilia misitu na ardhi katika juhudi za kupunguza na kuhimili mabadiliko ya tabianchi.