Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO bado kutangaza virusi vya Corona kama ni tishio la afya ya umma au la

Mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Geneva
Picha ya UN/Elma Okic
Mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Geneva

WHO bado kutangaza virusi vya Corona kama ni tishio la afya ya umma au la

Afya

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO limesema uamuzi kuhusu iwapo mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Corona nchini China  utangazwe kuwa dharura ya kimataifa ya umma unahitaji uchunguzi zaidi kabla ya kufanyika.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema hayo hii leo mjini Geneva, Uswisi baada ya kikao cha kamati ya dharura ya shirika hilo iliyokutana kutathmini hali halisi wakati huu ambapo tayari watu 9 wamethibitishwa kufariki dunia kutokana na ugonjwa huo.

“Uamuzi wa iwapo kutangaza au kutotangaza kuwa ni dharura ya kimataifa ya afya ya umm ani suala ambalo nalichukua kwa umakini sana na suala ambalo niko tayari kusema baada ya kuzingatia ushahidi wote,”  amesema Dkt. Tedros akizungumza na waandishi wa habari na kwa mantiki hiyo amesema, “timu yetu nchini China inashirikiana na wataalamu nchini humo na maafisa kuchunguza mlipuko huo. Tutakuwa na mengi zaidi ya kusema kesho.”

Dkt. Tedros amesema ameamua kuwa kamati hiyo ya dharura inayoongozwa na Dkt. Houssin ikutane tena kesho kuendelea na majadiliano na kamati imekubali.

Mkurugenzi Mkuu huyo wa WHO ametoa shukrani zake kwa ushirikiano kutoka Wizara ya afya ya China pamoja na uongozi wa Rais Xi Jinping na Waziri Mkuu kwa mchango wao na hatua walizochukua katika kukabiliana na mlipuko wa homa hiyo ya virusi vya Corona.

Kwa mujibu wa takwimu rasmi hadi jana jumanne ya tarehe 21  mwezi huu wa Januari mwaka 2020, majimbo 13 na manispaa nchini China yameripoti jumla ya wagonjwa 440 waliothibitishwa kuwa na homa  ya virusi vya Corona huku watu 9 wakiripotiwa kufariki dunia.

Japan nayo imeripoti mgonjwa mmoja aliyethibitishwa, nchini Thailand ni wagonjwa 3 na Korea Kusini mgonjwa mmoja.