Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kilimo cha “tangulia nakuja” sasa basi Kigoma

Wanawake wakipalilia kwenye moja ya mashamba darasa ya mahindi na maharagwe chini ya mpango wa pamoja mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Kigoma, KJP.
UN News/Assumpta Massoi
Wanawake wakipalilia kwenye moja ya mashamba darasa ya mahindi na maharagwe chini ya mpango wa pamoja mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Kigoma, KJP.

Kilimo cha “tangulia nakuja” sasa basi Kigoma

Tabianchi na mazingira

Katika mkoa wa Kigoma nchini Tanzania ambako Umoja wa Mataifa unatekeleza mpango wa pamoja kwa ajili ya mkoa huo, (Kigoma Joint Programme) kupitia mashirika yake ikiwemo lile la chakula na kilimo, FAO, matokeo chanya yameanza kudhihirika tangu kuanza kutekelezwa kwa mpango huo wenye maeneo kadhaa ikiwemo kilimo.

Miongoni mwa maeneo ambako mradi huo  unatekelezwa ni katika wilaya ya Kibondo ambako mratibu wa mpango huo wilayani humo, Martine Kapaya amemweleza Assumpta Massoi wa UN News Kiswahili kuwa mwaka jana walitekeleza mradi huo katika kata 7 na kufikia wakulima 2191 ambapo wakulima walipatiwa mafunzo ya kanuni bora za kilimo ikiwemo kuachana na upanzi wa kumwaga mbegu kiholela au tangulia nakuja na tayari wameshuhudia mabadiliko chanya akisema kwamba, "“Kuanzia ustawi wa mazao shambani hadi kwenye mavuno. Katika mashamba darasa ya mwaka jana mkulima alijionea alitumia kilo tatu za mbegu na akavuna kilo karibu 96 za maharagwe ambayo si kawaida wakati awali akiwa na ekari moja anapata magunia mawili ambayo ametumia karibu kilo 50 kwa sababu walikuwa na taratibu ya  kumwaga, walikuwa hawaamini kuwa maharagwe unaweza kupanda kwa nafasi , wanaamini kuwa maharagwe unaweza kuchukua na kutupa na kufukia na wanatumia mbegu nyingi halafu wanatumia mbegu za kienyeji unakuta anavuna magunia mawili badala ya manane au 12.”

Amesema kwa mwaka huu mradi  unatekelezwa katika kata nyingine 4 za Kizazi, Mabamba, Kumsenga na Busagala wakilenga kufikia wakulima 1914 na mwitikio ni mkubwa akisema kwamba, "wakulima wengi wamehamasika, katika matumizi ya mbegu hizo bora pamoja na mbolea. Kwa hiyo ukienda madukani mbolea na mbegu zimenunuliwa sana, hasa mbegu za mahindi, na mbolea hii ya kupandia na sasa hivi wananunua mbolea ya kukuzia. Kwa hiyo wakulima wengi wamehamasika sana. Pia kulikuwa na utaratibu wa kuwasogezea wakulima huduma za pembejeo kwa kuwauganishana wafanyabiashara. Mwitikio ulikuwa mkubwa, wakulima walikusanye hela na pembejeo zikawafikia huko vijijini. Waliona matokeo kupitia mashamba darasa. Kwa hiyo waliona mabadiliko pale akitumia mbegu yake ya kienyeji na akitumia mbegu zilizothibitishwa na taasisi zetu za utafiti , mbegu ambazo zinavumilia mabadilko ya tabianchi ambapo hata mvua zikipungua kidogo unaona mkulima anaweza kuvuna kuliko akitumia zile mbegu zake za zamani ambazo mvua ikipungua kidogo au jua likiwa kali amekosa kabisa na havuni.”

Mradi wa pamoja wa kwa ajili ya Kigoma, KJP una thamani ya dola milioni 47 na unahusisha mashirika 16 ya Umoja wa Mataifa ambapo utekelezaji wake unafanyika kwa ushirikiano na mamlaka za mkoa na wilaya kwa kuzingatia mahitaji ya mkoa huo ambao unahifadhi wakimbizi.

Mashirika hayo yanashirikiana kupitia maeneo saba ambayo ni nishati endelevu na mazingira, uwezeshaji vijana na wanawake, kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto, elimu ikijikita zaidi kwa wasichana barubaru, huduma za kujisafi au WASH, uendelezaji wa masoko na mpango wa afya, VVU na lishe.