Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jukwaa la kidijitali la kukusanya takwimu kuhusu njaa na mzozo duniani lazinduliwa:WFP

Ngala, jimbo la Borno zaidi ya watu milioni moja wakipokea mgao wa chakula na lishe kwa kaskazini mashariki mwa Nigeria mnamo Desemba 2016.
WFP/Amadou Baraze
Ngala, jimbo la Borno zaidi ya watu milioni moja wakipokea mgao wa chakula na lishe kwa kaskazini mashariki mwa Nigeria mnamo Desemba 2016.

Jukwaa la kidijitali la kukusanya takwimu kuhusu njaa na mzozo duniani lazinduliwa:WFP

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP leo limezindua jukwaa la kihistoria la kidijitali HungerMapLIVE, ambalo litakusanya takwimu muhimu kuhusu hali ya uhakika wa chakula katika nchi zaidi ya 90 duniani.

Kwa mujibu wa WFP takwimu za kila siku sio tu zitasaidia kupima kwa uhakika hali ya njaa bali pia zitasaidia kufanya maamuzi ya msingio nay a kuokoa maisha .

Jukwaa hilo “HungerMapLIVE” ni mfumo mpya wa kimataifa wa WFP wa kufuatilia na kutoa makadirio ya hali ya uhakika wa chakula kote duniani na kila mtu anaweza kupata fursa ya kuangalia kupitia wavuti hungermap.wfp.org.

Kuanzia leo jukwaa hilo HungerMapLive limeanza kufanyakazi. Limeandaliwa kwa ushirikiano wa WFP na kampuni ya ya kompyuta inayoongoza China ya Alibaba ijulikanayo kama Alibaba Cloud.

Mbali ya kwamba jukwaa hilo ni chanzo cha kupata tarifa kuhusu uhakika wa chakula , pia linatoa taarifa zingine muhimu kama masuala ya hali ya hewa, idadi ya watu, mizozo, lishe na hali ya majanga ya asili kama ukame.

Ikihimiza umuhimu wa jukwaa hilo WFP imesema “Ni jukwaa la mabadiliko, na ni nyenzo ambayo inatoa elimu kuhusu moja ya changamoto kubwa zaidi zinazoikabili dunia hivi sasa, njaa ya kimataifa. Kuwa na takwimu sahihi, za wakati muafaka katika hali yoyote inayoendelea ya mgogoro kunasaidia kuongeza fursa ya mafanikio ya kupambana na njaa.”

Kazi kubwa ya hungerMapLive

WFP inasema kipaumbele cha kwanza cha jukwaa hilo ni kuangazia watu walio na upungufu wa chakula katika nchi ambazo WFP inafanya operesheni zake na hasa katika nchi za kipato cha chini na cha wastani na kuruhusu kufahamu hali inavyobadilika siku hadi siku au mwezi hadi mwezi.

Hadi kufikia sasa WFP inasema zaidi ya watu bilioni moja ambao ni sawa na mtu 1 kati ya 7 duniani hawana chakula cha kutosha. Na hii inamaanisha kwamba hawana lishe ya kutosha au wako katika hatihati ya kutokuwa na uhakika wa chakula, na mbali ya kukosa chakula cha kutosha hawana uchaguzi wa lishe bora kwa ajili ya kuwa na maisha yenye afya.

Faida za HungerMapLive

Kwa kifupi jukwaa hili WFP inasema linaweza kusaidia kupunguza muda wa kukabiliana na majanga, kufanikisha operesheni, kupunguza gharama na kuziba pengo la taarifa katika jumuiya ya wahudumu wa misaada ya kibinadamu. Mbali ya kukusanya taarifa kutoka katika vyanzo mbalimbali vya umma kila siku , HungerMapLIVE inaweka mashine ya kujifunza ya akili bandia (AI) ili kutoa makadirio ya hali ya sasa ya uhakika wa chakula katika maeneo ambako takwimu ni vigumu kupata.