Mgonjwa mwingine wa virusi vya Corona abainika Korea Kusini; alitokea China

21 Januari 2020

Wakati idadi ya watu walioambukizwa ugonjwa wa Virusi vya Corona nchini China ikiripotiwa kufikia 205 na watu 3 wakifariki dunia nchini humo, Korea Kusini nayo imeripoti kisa cha kwanza cha mgonjwa ambaye ni raia China.

Shirika la afya ulimwenguni, WHO, kupitia taarifa yake iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi imesema kuwa mgonjwa huyo mwanamke mwenye umri wa miaka 35 anaishi Wuhan jimboni Hubei nchini China na aliwasili Korea Kusini akitokea China kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa Incheon.

WHO imesema mgonjwa huyo alipata  homa,  na maumivu ya misuli tarehe 18 mwezi huu wa Januari wakati bado akiwa nchini China na alisaka huduma ya  matibabu kwenye hospitali moja huko Wuhan ambako alibainika kuwa na mafua.

Punde baada ya kuwasili uwanja wa  ndege wa Incheon, mgonjwa huyo alipimwa na kubainika kuwa na virusi vya Corona.

Hata hivyo mgonjwa huyo amesema kuwa hakutembelea masoko yoyote ikiwemo soko la jumla la samaki huko Huanan wala hakuwa amekutana na mtu yeyote mwenye ugonjwa huo au kuwa na makaribiano na mnyama wa porini mwenye virusi hivyo.

Hatua zilizochukuliwa na Korea Kusini

Hivi sasa harakati zinaendelea kufuatilia watu wote waliokuwa karibu na mgonjwa huyo huku serikali ya Korea Kusini ikiimarisha kiwango cha tahadhari kutoka cha kwanza hadi cha 4.

Halikadhalika mamlaka za afya nchini Korea Kusini zimeimarisha harakati za ufuatiliaji wa ugonjwa wa vichomi tangu tarehe 3 mwezi huu wa Januari huku karantini na uchunguzi ukifanyika kwa wasafiri kutoka Wuhan.

Mtu anayeugua magonjwa ya njia ya hewa anashauriwa kuvaa barakoa kama aonekanavyo mwanamke huyu pichani,
Unsplash/Michael Amadeus
Mtu anayeugua magonjwa ya njia ya hewa anashauriwa kuvaa barakoa kama aonekanavyo mwanamke huyu pichani,

Tathmini na ushauri wa WHO

Kwa mujibu wa WHO, mgonjwa huyu wa sasa nchini Korea Kusini ni kisa cha nne kuripotiwa kuingizwa nchi jirani na msafiri kutoka mjini Wuhan nchini China.

Ni kwa mantiki hiyo WHO inashauri kuwa ni vyema jamii na wahudumu wa afya kuzingatia misingi ya kuepusha maambukizi zaidi ya magonjwa ya njia ya hewa kwa kuchukua hatua zifuatazo:

Mosi kuepuka kuwa karibu na watu wenye magonjwa ya njia ya hewa, pili kunawa mikono mara kwa mara hususan baada ya kuwa na makaribiano na wagonjwa, tatu, kuepuka kugusana na wanyama wafugwao au pori bila kuwa na vifaa vya kujikinga.

Halikadhalika watu wenye vikohozi wazingatie kujikinga pindi wanapokohoa badala ya kukohoa mdomo wazi.

Hata hivyo WHO imesema haina pendekezo lolote mahsusi kwa wasafiri isipokuwa kuwa tu makini iwapo msafiri atahisi kuugua ugonjwa wa njia ya hewa asake matibabu haraka iwezekanavyo.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter