Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa utafanya kila uwezalo kuwasaidia wakimbizi Za’atari:Lowcock

Wakimbizi wa Syria katika kambi ya Za'atari nchini Jordan.
UNICEF/Christopher Herwig
Wakimbizi wa Syria katika kambi ya Za'atari nchini Jordan.

Umoja wa Mataifa utafanya kila uwezalo kuwasaidia wakimbizi Za’atari:Lowcock

Msaada wa Kibinadamu

Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura, OCHA, Mark Lowcock amezuru moja ya kambi kubwa zaidi ya wakimbizi nchini Jordan ya Za’atari kujionea hali halisi na kuzungumza na wakimbizi kutoka Syria. 

Kambini Za’atari, wakati wa ziara ya Bwana Lowcock katika kambi hii inayohifadhi wakimbizi 76,000 wanawake, watoto na wanaume ni sehemu ya ziara yake nchini Jordan ambako amekutana na watu mbalimbali wakiwemo maafisa wa serikali na pia kupokea tarifa kutoka kwa kamanda mkuu wa jeshi la Jordan.

Lowcock ameiahidi serikali ya Jordan kuwa Umoja wa Mataifa utahakikisha msaada unaendelea kwa nchi hiyo ili iweze kumudu mzigo mkubwa wa wakimbizi hasa kutoka Syria amesema, “Umoja wa Mataifa utafanya kila tuwezalo kuhakikisha kwamba jumuiya ya kimataifa inaendelea na msaada wake kwa Jordan. Na asante kwa kunipa fursa ya kuzuru.”

 Kwenye kambi ya Za’atari amekutana na familia za wakimbizi wa Syria na wafanyakazi wa mashirika mbalimbali ya misaada ya kibinadamu kambini hapo.

Akiwa kambini hapa ametembelea pia kituo cha jamii na kuzungumza na wakazi mbalimbali, na baada ya hapo akajionea kazi za sanaa za uchoraji zilizofanywa na wakimbizi kambini Za’atari.

Bwana Lowcock alikwenda pia kuzuru shule ambako watoto wakimbizi wa Syria wanajumuishwa katika mfumo wa elimu wa Jordan.

Kabla ya kuwasili Za’atari Bwana Lowcock alikutana na maafisa wa serikali, wanadiplomasia, mashirika ya kitaifa na kimataifa yasiyo ya kiserikali au NGO’s na mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayohusika na masuala ya kibinadamu kukabiliana na zahma ya mgogoro wa Syria.

Kati ya jumla ya Wasyria milioni 5.6 waliofungasha virago na kuikimbia nchi yao tangu kuanza kwa vita 2011, takribani 650,000 wako Jordan na hivyo kuifanya nchi hiyo kuwa ni ya tatu hivi sasa duniani kwa kubeba na kuhifadhi mzigo mkubwa wa wakimbizi wa Syria.