Takribani watu nusu bilioni hawawezi kupata ajira zenye hadhi, kukosekana kwa ajira kunaongezeka-ILO

20 Januari 2020

Takribani  nusu ya watu bilioni moja wanafanya kazi saa chache za kulipwa kuliko zile ambazo wangependa au kukosekana kabisa kwa kazi za kulipwa. Hiyo ni kwa mujibu wa riupoti mpya ya shirika la kazi duniani.

Aidha, ripoti hiyo kwa jina Ajira ya dunia na mtazamo wa jamii: mwenendo wa mwaka 2020 au WESO, inaonesha kuwa kukosekana kwa ajira kunategemewa kuongezeka kwa karibia na watu milioni 2.5 katika mwaka huu wa 2020.

Hali ya kukosekana kwa ajira duniani kumesalia katika hali isiyoongezeka kwa miaka tisa lakini kumezorotesha ukuaji wa uchumi inaamaanisha kuwa kwa kadiri nguvu kazi inavyoongezeka, hakuna kazi mpya za kutosha zinazozalishwa kuweza kupokea watu wapya wanaoongia katika soko la ajira.

Guy Ryder, Mkurugenzi Mkuu wa ILO akiizungumzia ripoti hiyo hii leo Januari 20, mjini Geneva Uswisi amesema, “watu wa umri mdogo wanakabiliwa na changamoto fulani za soko la kazi. Na kuna takwimu za kushangaza katika ripoti hii, ni kuwa asilimia 22 za vijana wadogo, 267 kati yao wako katika kundi linalofahamika kama NEET yaani ambao hawako katika ajira, hawako katika elimu na mafunzo. N a hivyo hii ni, nafikiri, moja ya changamoto za wakati wetu.”

Ryder pia amesema, “jinsia, bila shaka ndiyo Ryder ni mwelekeo mkubwa katika ukosefu wa usawa. Katika mwaka wa 2019, ushiriki wa nguvu kazi ya wanawake ulikuwa asilimia 47, na hiyo ni asilimia 27 chini ya kiwango cha wanaume."

Ripoti hiyo imeendelea kuonesha kuwa kukosekana kwa ulinganifu kati ya kazi na uhitaji inaenda zaidi ya kukosekana kwa ajira hadi kwenye kutokutumia vya kutosha nguvu kazi iliyopo.  Aidha, katika nyongeza ya idadi ya kidunia ya watu wasio na ajira ambayo ni milioni 188, watu milioni 165 hawana kazi za kutosha kulipwa na watu milioni 120 ni ama wamekata tamaa kuendelea kutafuta kazi au hawana nafasi ya kuingia katika soko la ajira. Jumla, zaidi ya watu milioni 470 kote duniani wameathirika.

Ryder amesisitiza kuwa ni muhimu kwamba ripoti hii “inaenda zaidi ya kusema tu kukosekana kwa ajira duniani ambayo inasalia katika asilimia 5.5 yaani watu milioni 188. Inaenda mbali zaidi kuangazia ni kwa kiwango ambacho tunakiita nguvu kazi ambayo haijatumika ipasavyo.”

Amefafanua, “hawa ni watu ambao hawajaajiriwa rasmi, si sehemu ya wale milioni 188, lakini watu ambao pengine hawafanyi kazi saa nyingi kwa kadri ambavyo wangependa kufanya kazi. Huu ni muda ambao hautumiki vya kutosha. Watu ambao wapo tayari kwa ajili ya kazi lakini pengine wamekata tamaa ya kuendelea kujaribu. Au watu ambao tayari wameanza kutafuta kazi, hata kama hii leo hawapo kwa ajili ya kazi hiyo.”

Mkurugenzi Mkuu wa ILO ameendelea kusema, “kwa hivyo hii ni nguvu kazi. Na hii ndio hoja: ikiwa ukijumlisha makundi yote hayo pamoja, unapata asilimia 5.4 ya ajira za wazi kwa asilimia 13 ya nguvu kazi duniani ambao kwa namna moja ama nyingine hawajatumika vya kutosha.”

Ryder ameongeza pia kuwa, “tuna tatizo kubwa la kuzalisha fursa za ajira bora. Na tatizo hilo pengine ni kubwa kuliko vile tunavyotambua kwa kuangazia katika takwimu za ukosekanaji wa ajira.”

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter