Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uvutaji tumbaku unaongeza hatari ya madhila baada ya upasuaji:WHO

Mwanaume akivuta sigara katika eneo lililotengwa kwa ajili ya wavuta sigara kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York Marekani.
UN News/Yasmina Guerda
Mwanaume akivuta sigara katika eneo lililotengwa kwa ajili ya wavuta sigara kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York Marekani.

Uvutaji tumbaku unaongeza hatari ya madhila baada ya upasuaji:WHO

Afya

Wavutaji wa bidhaa za tumbaku wako katika hatari kubwa ya kupata madhila zaidi baada ya kufanyiwa upasuaji kuliko wasiovuta bidhaa hizo limeonya shirika la afya duniani WHO.

Kwa mujibu wa taarifa ya shirika hilo iliyotolewa leo miongoni mwa hatari hizo ni matatizo ya moyo na mapafu kushindwa kufanya kazi ipasavyo, maambukizi na kuchelewa kupona kwa mshono.

Taarifa hiyo imesema lakini ushahidi mpya umeonyesha kwamba watu ambao wanaacha kuvuta bidhaa za tumbaku wiki nne au zaidi kabla ya kufanyiwa upasuaji hatari ya kupata matatizo mengine zaidi baada ya upasuaji inapungua na kuwa na matokeo mazuri miezi sita baadaye.

WHO imesema wagonjwa ambao huacha kabisa kuvuta bidhaa za tumbaku wana afueni ya kutopata matatizo wanapopatiwa dawa ya usingizi wakati wa upasuaji ikilinganishwa na ambao bado wanavuta.

Taarifa hii imetokana na utafiti wa pamoja wa WHO, Chuo kikuu cha Newcastle, Australia na shirikisho la watoa dawa za usingizi duniani (WFSA).

Dkt. Vinayak Prasad mkuu wa kitengo cha kupinga matumizi ya tumbaku kwenye shirika la WHO amesema utafiti huo unaonyesha kwamba kila anayeishi bila kuvuta tumbaku kwa kila wiki , baada ya wiki nne anaboresha afya yake kwa asilimia 19. “Ripoti ya utafiti inatoa ushahidi kwamba kuna faida za kuahirisha upasuaji usio wa dharura na kuwapa wagonjwa fursa ya kuacha kuvuta sigara , na hivyo kuwa na matokeo mazuri zaidi ya kiafya.”

Ameongeza kuwa nikotini na carbon Monoxide vinavyopatikana kwenye sigara vinaongeza hatari ya matatizo ya moyo baada ya upasuaji.

Uvutaji wa tumbaku pia unaathiri mapafu na kufanya kuwa vigumu hewa inayostahili kuingia mwilini na kuongeza hatari baada ya upasuaji.

Naye mratibu wa WHO kuhusu ubora wa huduma Dkt Shams Syed amesema “Matatizo baada ya upasuaji yanaongeza mzigo kwa watoaji wa huduma za afya na kwa mgonjwa. Wataalam wa afya, madaktari wa upasuaji, wauguzi na familia ni muhimu sana kumsaidia mgonjwa kuacha uvuitaji sigara katika hatua zote za hudumahususan kabla ya upasuaji”

WHO inazichagiza nchi kujumuisha program za uchagizaji wa kuacha uvutaji  na kampeni ya elimu katika mifumo ya afya ili kuelimisha na kusaidia watu kuacha uvutaji bidhaa za tumbaku.