Katibu Mkuu wa 5 wa UN Perez de Cuellar atimiza miaka 100

Salamu za pongezi ya siku ya kuzaliwa zimetumwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa 5 wa Umoja wa Mataifa Javier Pérez de Cuéllar kwa kuadhimisha miaka 100 ya kuzaliwa.
Pérez de Cuéllar raia wa Peru ambaye alihudumu mihula miwli kwenye Umoja wa Mataifa miaka ya 1980, Katibu Mkuu wa sasa Guterres amesema alikuwa mchapa kazi na hata katika siku ya mwisho ya wajibu wake kama Katibu Mkuu alihakikisha amefanikisha juhudi za kihistoria kwa kutiwa saini mkataba wa amani ambao ulimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mingi nchini El Salvador.
Pérez de Cuéllar ambaye kitaaluma ni mwanasheria tangu mwaka 1940 katika maisha yake ameshika nyadhifa mbalimbali za kidiplomasia kuanzia kwenye wizara ya mambo ya nje na kwenye Umoja wa Mataifa.
De Cuellar aliwahi kuwa balozi wa Peru nchini Uswisi, Kwenye Muungano wa Soviet, Poland na Venezuela.
Kama miongoni mwa wajumbe wa Peru alishiriki kikao cha kwanza cha Baraza Kuu mwaka 1946. Na akawa mwakilishi wa kudumu wa Peru kwenye Umoja wa Mataifa mwaka 1971 na kuanzia hapo ni kama hakuondoka kwenye Umoja wa Mataifa.
Mwaka 1975 Pérez de Cuéllar aliteuliwa kuwa mwakilishi wa Katibu Mkuu nchini Cyprus na kushika nyadhifa nyingine mbalimbali mpaka Desemba 1977 na miaka miwili baadaye alichukua wadhifa wa msaidizi maalumu wa Katibu Mkuu kwa masuala ya kisiasa.
Na kuanzia April mwaka 1981 alihudumu kama mwakilishi wa Katibu Mkuu katika kutatua mgogoro wa Afghanistan na hata aliporejea kufanya kazi kwenye wizara ya mambo ya nje ya Peru, Pérez de Cuéllar aliendelea kumuwakilisha Katibu Mkuu katika masuala ya Afghanistan.
Baada ya kuchukua madaraka rasmi kama Katibu Mkuu wa 5 wa Umoja wa Mataifa tarehe 01 Januari 1982 miezi michache baadaye katika ripoti yake ya kwanza kuhusu kazi za shirika, kiongozi huyo alitoa tathimini kali ya iliyokosoa vikali, kwa mujibu wake wakati huo Baraza la Usalama “haliwezi kuchukua maamuzi ya hatua za lazima kutatua migogoro ya kimataifa. Na hata maamuzi hayo yanapofanyika matarajio ya utekelezaji wake katika mazingira ya mgawanyiko kwenye jumuiya ya kimataifa ni sufuri.”
Kipaumbele chake kilikuwa kuubadilisha Umoja wa Mataifa kuwa shirika linaloweza kutimiza majukumu yake ya kuhakikisha amani na usalama. Pérez de Cuéllar alisema “Endapo hili halitofanyika jumuiya ya kimataifa itakuwa kazi bure katika masuala ya migogoro ya kijeshi ambayo inatishia msingi wa amani ya kimataifa.”
Akiondoka madarakani kama Katibu Mkuu wa 5 wa Umoja wa Mataifa katika majira ya kiangazi mwaka 1991 Pérez de Cuéllar alitoa ripoti yake ya mwisho ambayo ilikuwa tofauti na ya kwanza safari hii aliandika kuhusu kufufua Umoja wa Mataifa, kumaliza mkwamo wa muda mrefu. Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo wa 5 “Umoja wa Mataifa ulikuwa ukienda sanjari na mabadiliko ya haraka ya kihistoria katika miaka ya karibuni na ulipata mafanikio makubwa katika ulinzi wa amani.” Licha ya kukosolewa hapa na pale mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alisema “Hakuna mtu anayeweza kuongeza mara mbili utendaji wa Umoja wa Mataifa . Umoja wa Mataifa unaingia katika zama mpya na unachukua majukumu ambayo hayakuwepo kwenye mipango ya awali ya kuanzishwa kwa Umoja huu.”
Kama anavyoendelea kusisitiza Katibu Mkuu wa sasa Antonio Guterres leo hii Dunia imeingia tena katika zama mpya za maendeleo yake, mambo yamebadilika na migawanyiko imeongezeka, pengo la kutokuwepo kwa usawa linazidi kupanuka likichangiwa na utandawazi usio sawia, ugaidi, na hata mabadiliko ya tabianchi. Yote haya yanahitaji suluhu bunifu. Katika kumpongeza Javier Pérez de Cuéllar Katibu Mkuu Guterres amekumbusha kwamba kila mtu anayefanya kazi kwenye Umoja wa Mataifa ambao unaadhimisha miaka 75 mwaka huu atakumbuka sifa nzuri ya Katibu Mkuu Pérez de Cuéllar na hasa imani yake katika Umoja wa Mataifa .
Akimnukuu amesema “Hakuna magumu yaliyo mbele yetu ambayo yatadunisha umuhimu wa yale Umoja wa Mataifa uliyoyapitia” akiandika katika ripoti yake ya karibuni kuhusu kazi za shirika hili “kuzaliwa upya kwa shirika hili ni ushahidi tosha ya utu wa ubinadamu”.