Hali ya maelfu ya watoto wakimbizi na wahamiaji Libya inasikitisha:UNICEF

17 Januari 2020

Dunia haipaswi kukubali hali mbaya na isiyoelezeka inayowakabili maelfu ya watoto wakimbizi na wahamiaji nchini Libya amesema mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.

Katika taarifa yake iliyotolewa leo Ijumaa Bi. Henrietta Fore amesema “watoto nchini Libya wakiwemo wakimbizi na wahamiaji wanaendelea kulipa gharama kubwa wakati vita vya wenyewe kwa wenyewe vikiendelea nchini humo.”

Tangu mwezi Aprili mwaka jana mapigano mapya yalipozuka nnje ya mji mkuu Tripoli na Magharibi mwa Libya hali ya maelfu ya watoto na raia imeendelea kuzorota huku mashambulizi katika maeneo yenye idadi kubwa ya watu yakisababisha majeruhi na vifo vya mamia ya watu.

Kwa mujibu wa Bi. Fore UNICEF imepokea ripoti za watoto kulemazwa, kuuawa na kuingizwa jeshini kupigana. Tangu kuangushwa utawala wa Rais Muammar Gaddafi mwaka 2011 Libya imekuwa katika machafuko, kukosa utulivu na uchumi kuporomoka licha ya kuwa na akiba kubwa ya mafuta.

Maelfu ya watu wameuawa katika mapigano baina ya jeshi la serikali ya Libya iliyojitangaza  LNA linaloongozwa na kamanda Khalifa Haftar lililojikita katika eneo la Mashariki mwa nchi na serikali ya Tripoli inayotambulika na Umoja wa Mataifa iliyojikita katika uapnde wa Magharibi.

Katibu Mkuu Antonio Guterres atahudhuria mkutano mkubwa wa kimataifa unaotarajiwa kufanyika Jumapili nchini Ujerumani ambapo waziri mkuu anayetambulika na Umoja wa Mataifa  na kamanda Haftar wanatarajiwa kuhudhuria kwa matumaini ya kukomesha mapigano moja kwa moja.

Wakati huohuo UNICEF inasema katika kipindi cha miezi minane iliyopita zaidi ya watu 150,000 wakiwemo watoto 90,000 wamelazimika kufungasha virago na kukimbia makwao na sasa ni wakimbizi wa ndani.

Uharibifu mkubwa

Bi. Fore pia ametaja kwamba mashambulizi haya pia ymekumba  mioundombinu muhimu ambayo watoto wanaitegemea kwa ajili ya kuishi na mustakabali wao. “Karibu vituo 30 vya afya viaharibiwa wakati wa mapigano haya na 13 kati ya hivyo kulazimika kufungwa. Mashambulizi dhidi ya shule na tishio la machafuko vimesababisha shule nyingi kufungwa na kuwaacha watoto takribani 200,000 kutohudhuria masomo.”

Zaidi ya hayo amesema mifumo ya maji imeshambuliwa na udhibiti wa mfumo wa maji taka umesambaratika na hivyo kuongeza hatari ya maradhi ya kuambukiza yatokanayo na maji ikiwemo kipindupindu.

“watoto wakimbizi na wahamiaji 60,000 walioko katika maeneo ya mijini hivi sasa wako katika hali mbaya na hatari kubwa, hususani watoto 15,000 ambao hawana walezi au wazazi na wale ambao wanashikiliwa katika vizuizini. Watoto hawa tayari walikuwa hawapati fursa ya kutosha ya ulinzi na huduma za msingi hivyo kushika kasi kwa machafuko pia kumezidisha hatari inayowakabili.”

Utoaji msaada UNICEF na washirika wake katika maeneo hayo wanawasaidia watoto  na familia zao kupata huduma za afya na lishe, ulinzi, elimu, maji na usafi.

Fikieni muafaka wa amani wa kudumu kwa maslahi ya kila mtoto nchini Libya-Mkuu wa UNICEF

UNICEF pia inawafikia watoto wakimbizi na wahamiaji kwa misaada ikiwemo wale wanaoshikiliwa katika vituo mbalimbali.  “Chakusikitisha ni kwamba mashambulizi dhidi ya maeneo ya raia yaliyo na watu wengi na miundimbinu yao,  pia dhidi ya wahudumu wa misaada ya kibinadamu na wahudumu wa afya vinaathiri juhudi za misaada ya kibinadamu.”

Bi. Fore ametoa wito kwa pande zote kinzani katika mzozo huo na kwa wale walio na ushawishi n apande hizo kuwalinda watoto, kuacha kuwatumia na kuwaingiza watoto jeshini , kusitisha mashambulizi dhidi ya raia na miundombinu yao na kuruhusu fursa ya bila vikwazo ya kuwafikia watoto na misaada ya kibinadamu na pia watu wengine wenye uhitaji.”

Pia ametoa wito kwa mamlaka ya Libya kuacha kuwaweka vizuizini watoto wahamiaji na wakimbizi na kusaka njia mbadala ambayo ni salama na ya kiutu.

Kabla ya mkutano wa amani mjini Berlin Jumapili Bi. Fore amezitaka pande zote katika mzozo na watu wenye ushawishi juu ya pande hizo “Kufikia haraka muafaka wa kudumu na wa kina wa amani kwa ajili ya maslahi ya kila mtoto nchini Libya.”

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter