Mangariba watupa visu vya ukeketaji Sierra Leone

20 Januari 2020

Mangariba zaidi ya 60 nchini Sierra Leone  maarufu kama Soweis wamekata shauri na kuvitelekeza visu vyao walivyovitumia miaka nenda miaka rudi kukeketa maelfu ya wanawake na wasichana.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake UN Women, nchini Sierra Leone takriban wanawake 9 katik ya 10 wamekeketwa kama sehemu ya utamaduni wa kuwa mwanamke kamili.

Ukeketaji mzizi wake ni ubaguzi wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana na unaweza kuwa na athari mbaya sana za kiafya na hata kusababisha vifo.

Na kutokana na kampeni kubwa iliyofanywa na UN Women  nchini humo katika hatua ya kutia matumaini mwishoni mwa Desemba mwaka 2019 mangariba zaidi ya 60 wameamua kuachana kabisa na mila hiyo haramu ya ukeketaji na kutupa visu vyao huku wakiahidi kutoirejea tena. Dkt. Mary Okumu ni mwakilishi wa UN Women nchini Sierra Leone

(SAUTI YA MARY OKUMU)

“Tuko katika wakati muhimu katika historia, mangariba ambao hufanya ukeketaji huo katika hafla ya wazi wametangaza na kuachana kabisa na FGM”

Agnes Kanu mmoja wa mangariba nchini humo anasema ndio wamekomesha ukeketaji na wasicha hawakatwi tena lakini mila zingine zote zinaendelea.

Naye Rugiatu Neneh Turay mwanzilishi wa mradi wa Amazon wa kupambana na ukeketaji nchini humo anasema jitihada za pamoja ndizo zilizofanikisha hatua hiyo

(SAUTI YA RUGIATU NENEH)

“Kina mama , mangariba, na jamii wote tumekuja pamoja katika mchakato huu na tutaendelea kusambaza ujumbe wa kuleta mabadiliko.”

Kwa mujibu wa UN Women hii ni hatua kubwa inayopaswa kuigwa na mangariba wengine wote popote walipo duniani.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud