Ripoti ya “Wamefuta ndoto za watoto wangu” yachapishwa nchini Syria

16 Januari 2020

Ripoti ya tume ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Syria imesema katika Jamhuri ya kiarabu ya Syria, watoto   wameporwa utoto wao kwa kulazimishwa kushiriki katika vita ya kikatili na pia kumekuwa na ukiukwaji wa haki zao kutoka katika pande zote za mzozo huku wakibaki katika katika hatari ya dhuluma na unyanyasaji.

Katika ripoti hiyo yenye kurasa 25 iliyotolewa leo ikiwa na jina “Wamefuta ndoto za watoto wangu,” tume ya watu watatu imetaja ukiukwaji kadhaa wa haki za watoto ikiwemo zaidi ya watoto milioni 5 kutawanywa ndani na nje ya nchi na jinsi ambavyo wavulana kwa wasichana walivyoporwa utoto wao kati vita katili iliyodumu kwa miaka nane na nusu.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi, Paul Pinheiro amesema,  “ninasikitishwa na kudharauliwa kwa sheria za vita na mkataba wa haki za watoto kunakofanywa na pande zote zinazohusika katika mzozo. Wakati serikali serikali ya Jamhuri ya kiarabu ya Syria ina jukumu la msingi la kulinda wavulana na wasichana wa nchi hiyo, wahusika wote katika mzozo huu wanapaswa kufanya zaidi kuwalinda watoto na kuhifadhi kizazi kijacho cha nchi hiyo.”

Ripoti hiyo iliyofuatilia kipindi cha kati ya Septemba 2011 hadi mwisho wa mwezi Oktoba 2019 imeendelea kueleza kuwa watoto wameuawa na kulemazwa na kukabiliwa na ukiukwaji mkubwa kutoka katika pande zinazokinzana.

Mara kadhaa, vikosi vinavyoiunga mkono serikali vilitumia mabomu na kemikali zinazosababisha majeraha na vifo kwa watoto.  Ubakaji na pia unyanyasaji wa kijinsia vimekuwa vikitumika mara kwa mara dhidi ya wanaume na wanawake, wavulana na wasichana ikiwa ni kama njia ya kuwaadhibu, kudhalilisha na kusababisha hofu miongoni mwa jamii. Vikosi vya serikali vimewakamata watoto wavulana wa umri wa miaka 12, kuwashambulia vibaya na kuwatesa.

Tangu kuanza kwa mgogoro, maelfu ya shule yameharibiwa au kutumiwa kwa malengo ya kijeshi na zaidi ya wavulana na wasichana milioni 2.1 hawahudhurii madarasa ya namna yoyote.

Makundi yenye silaha yamekuwa yakizilenga shule. Na madhara ya mgogoro kwa afya ya akili na mwili imeendelea kuwa mbaya zaidi.

Miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa na tume kwa serikaali ya Syria na wadau wengine wanaohusika na mgogoro huu ni kuboresha ulinzi kwa watoto kwa kuzingatia sheria za kimataifa na haki za watoto.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud