Unapokuwa mkimbizi huchoki kuota ndoto:Wakimbizi Bidibidi Uganda

16 Januari 2020

Unapokuwa mkimbizi huchoki kuota ndoto za siku moja maisha yako yatabadilika na kuachana na jinamizi lililolazimisha kufungasha virago.  Hii ni kauli ya baadhi ya wakimbizi kutoka Sudan Kusini ambao hivi karibuni wamepatiwa mafunzo na shirika la mpango wa chakula duniani WFP kuhadhithia maisha ya ukimbizini. 

Katika makazi ya wakimbizi ya bidibidi nchini Uganda wakimbizi 34 kutoka Sudan Kusini wanajiandaa katika mafunzo ya WFP ya kuwa wahadithiaji wa Habari za wakimbizi kwa njia ya kidijitali.

Katika mafunzo hayo ya wiki mbili wakimbizi hawa wanajifunza mengi ikiwemo kupiga picha nzuri, kurekodi video na kuchapisha hadithi zao kwenye mitandao ya kijamii kama Facebook na Instagram ili dunia iweze kuziona na kuzisikia hadithi zao. Malishi ni mmoja wa wakimbizi hao wanaopatiwa mafunzo

(SAUTI YA MALISH)

“Nataka watu wasikie sauti yangu na nataka kuwapa watu hadithi hizi, nataka kuwapa hadithi zangu mwenyewe na za watu wengine, kuna baadhi ya vitu katika nchi yangu ambavyo havijulikani nje, hivyo nataka watu wa nje wavifahamu, ili dunia nzima ivijue”

Wakielekea darasani kwenye mafunzo hayo mkufunzi kutoka WFP Rosebell Kagumire yuko tayari

(SAUTI YA ROSEMBELL KAGUMIRE)

“Mimi ni mwandishi na mwanablogu, hawa ni vijana wakimbizi na nimekuwa sehemu ya timu ya kuwafunza ujuzi wa kutambua kwamba wana hadithi , na wanaweza kusimulia hadithi zao sio lazima wasubiri waandishi wa Habari kuzungumza nao, sio lazima wasubiri mtu yeyote au mashirika wakati wana ujuzi huu,wanaweza kutumia simu zao za rununu, kwani katika zama hizi kila mtu anaweza kusimua hadithi yake.”

Mafunzo hayo ni mchakato unahitaji dhamira, jitihada na vipaji mbalimbali vya kusimulia hadithi hizo. Wengine kama Spike wameamua kutumia muziki wa kufokafoka kueleza kilicho moyoni

Na wanawake ambao mara nyingi huachwa nyuma katika mafunzo haya ya WFP  wamepewa kipaumbele kwa kuwa wana mengi ya kueleza akiwemo Eva

(SAUTI YA EVA)

“Sio wavulana tu wanaoweza kupata hadithi, lakini hata wasichana wanaweza kupata hadithi, kuna wasicha wadogo ambao wanakabiliwa na changamoto kambini , na kuna wasichana wadogo ambao wanaendesha familia , hivyo ni muhimu sana kwetu kuieleza dunia kuhusu hayo.”

WFP inatumai kwamba mafunzo haya na hadithi za wakimbizi zinazosimuliwa vitakuwa taa ya kuangazia mahitaji yao, Maisha yao na madhila waliyopitia.

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter