Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shule ya kwanza ya mafunzo ya ndege zisizo na rubani na takwimu yafunguliwa Afrika-UNICEF

Wanakijiji wilayani Kasungu nchini Malawi waangalia onyesho la kukimbia kwa ndege inayoruka bila rubani
UNICEF/Andrew Brown
Wanakijiji wilayani Kasungu nchini Malawi waangalia onyesho la kukimbia kwa ndege inayoruka bila rubani

Shule ya kwanza ya mafunzo ya ndege zisizo na rubani na takwimu yafunguliwa Afrika-UNICEF

Ukuaji wa Kiuchumi

Shule ya kwanza ya mafunzo kuhusu ndege zinazoruka bila rubani (Drone) na takwimu, ADDA imefunguliwa Lilongwe, nchini Malawi Januari 13 mwaka 2020 limesema Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.

Hatua hiyo ni katika juhudi za kuimarisha matumizi ya ndege zinazoruka bila rubani katika programu na huduma ambazo zitaathiri maisha ya watoto na vijana.

Akizungumzia uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF, Henrietta Fore amesema, “programu za misaada ya kibinadamu na maendeleo barani Afrika zinaweza kunufaika kwa kiasi kikubwa kutokana na matumizi ya teknolojia ya ndege zinazoruka bila rubani.”

Ameongeza kwamba, “shule ya Afrika ya ndege zinazoruka bila rubani na takwimu itakuwa na mchango mkubwa katika kuwajengea vijana stadi wanazozihitaji katika kutumia teknolojia hiyo kwa ajili ya watoto wao na jamii.”

Katika kuendeleza kazi ya misaada ya kibinadamu Afrika shule hiyo iliyozinduliwa Malawi itaimarisha ustadi wa matumizi ya ndege hizo kwa ajili ya shughuli za kibinadamu, maendeleo na biashara barani Afrika kupitia mafunzo ya wiki 12 ambapo inakadiria kutoa mafunzo wa wanafuzni takriban 150 kujenga na kurusha ndege zinazoruka bila rubani kufikia mwaka 2021.

Ufadhili kutoka kwa wadau wa UNICEF kutatoa fursa kwa wanafunzi 26 kutoka Afrika kusoma bila malipo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kitengo cha Shirika la maswala ya anga, James Chakwera amesema, “Malawi tunaamini kwamba kukumbatia teknolojia za kisasa kwa mfano ndege zinazoruka bila rubani na tathmini bora ya takwimu na usimamizi kutatusaidia kuhudumia watoto wetu. Tunafuraha kuungana na UNICEF katika ushirkiano huu mzuri.”

Mtaala umetengenezwa kwa ushirikiano na taasisi ya mafunzo ya Virginia na Chuo Kikuu chaVirgina kufuatia warsha zao za mafunzo nchini Malawi tangu 2017 ambapo mafunzo yatajumuisha mafunzo darasani na matendo ikiwemo ya kukarabati na kurusha ndege hizo.

Kufikia mwaka 2022 ADDA itaendesha programu ya shahada ya uzamili kuhusu teknolojia ya ndege zinazoruka bila rubani ya miaka miwili bila malipo kwa ushirikiano na chuo cha Malawi cha sayansi na teknolojia.