Wahamiaji elfu moja warejeshwa Libya baada ya kufunga safari kuvuka Mediterranea-IOM

14 Januari 2020

Takriban wahamiaji elfu moja ikiwemo zaidi ya wanawake mia mbili na watoto wamerejeshwa katika pwani ya Libya tangu kuanza kwa mwaka huu limesema Shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM.

Akizungumza na waandishi wa habari, mjini Geneva, Uswisi, msemaji wa IOM Safa Msehli amesema wengi wametua Tripoli wakati mzozo wa makundi yaliyojihami ukiendelea mji mkuu na wamepelekwa moja kwa moja vizuizini.

Bi Msehli amewaambia waandishi wa habari kwamba, “wahamiaji hawa waliorejeshwa ni miongoni mwa elfu moja walioondoka Libya kwa njia ya bahari tangu Januari Mosi kufuatia mapigano makali Tripoli yaliyozuka miezi tisa iliyopita.”

Ameongeza kwamba, “wahamiaji waliozungumza na wafanyakazi wa IOM katika maeneo wanakowasili nchini Libya wamesema ongezeko la uhasama ndani na karibu mwa mji mkuu na hali inayoendelea kuzorota ya kibinadamu ni sababu kubwa za ongezeko la safari hizo za kuondoka wahamiaji.”

Ikilinganishwa na kipindi kama hiki mwaka jana miili 23 ilipatikana na walinzi wa pwani ya Libya na hakuna wahamiaji waliorejeshwa Libya. Hali ya sasa ya ongezeko la watu wanofunga safari imetajwa na IOM kama ya kusikitisha ukizingatia uwezo mdogo wa kutafuta na kuokoa watu katika bahari ya Mediterranea.

Timu ya IOM wanatoa msaada wa dharura kwa wahamiaji katika vituo vya kuwasili ikiwemo huduma ya afya na uchunugzi lakini shirika hilo linasema mikakati ya kulinda maisha na kuhakikisha usalama wa wahamiaji wanaorejeshwa wakijaribu kukimbia hali mbaya Libya bado haijashughulikiwa.

Msemaji huyo wa IOM amesema IOM imekuwa ikitoa wito wa kusambaratishwa kwa mfumo huo wa kuzuia na kuachiwa huru wahamiaji kwa utaratibu na kwamba njia mbadala zinazolinda Maisha lazima zipatikane kwa ajili ya kuondoa madhila kwa maelfu ya wanaume, wanawake na watoto wanaoshikiliwa katika mazingira yasiyozingatia utu.

Takriban wahamiaji elfu moja walijiandikisha kurejea kwa hiari na program ya IOM wamekwama Libya kutokana na hali mbaya ya kiusalama nchini. Hali mbaya ya kiusalama mji mkuu Libya imekwamisha shughuli za safari za anga na kukwamisha shughuli muhimu za kuokoa maisha.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter