Mauaji ya watetezi wa haki za binadamu Colombia yanatutia hofu kubwa:UN

14 Januari 2020

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa (OHCHR) imesema inatiwa wasiwasi mkubwa na idadi ya watetezi wa haki za binadamu waliouawa nchini Colombia mwaka 2019.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na msemaji wa ofisi hiyo Marta Hurtado mjini Geneva Uswis takwimu zinaonyesha kwamba wanaharakati 107 waliuawa mwaka jana na ofisi ya haki za binadamu nchini Colombia iko katika mchakato wa kubaini visa vingine 13 zaidi vilivyoripotiwa mwaka 2019 na kama vitathibitika kuwa kweli badi watetezi wa haki za binadamu waliouwa mwaka jana Colombia watafikia jumla ya 120.

Taarifa hiyo imeongeza kwamba “Mashambulizi dhidi ya watetezi wa haki za binadamu tayari yalikuwa yameongezeka tangu mwaka 2018 ambapo ofisi ya haki za binadamu ilithibitisha kuuawa kwa watu 115 mwaka huo. Huu ni mwenendo mbaya na hauonyeshi kupungua mwaka huu 20202 ambao tayari watetezi 10 wa haki za binadamu wamesharipotiwa kuuawa katika siku 13 za kwanza za mwezi huu wa Januari.”

Ofisi hiyo ya haki za binadamu imerejelea wito wake kwa serikali ya Colombia kufanya juhudi kuzuia mashambulizi haya dhidi ya watetezi wa haki za binadamu, kuchunguza kila kisa na kuwawajibisha wahusika ikiwemo waliochochea, kusaidia na kuchagiza ukiukwaji huo wa haki za binadamu. “Mwenendo huu una mzunguko huu wa mauaji , machafuko na ukwepaji sheria lazima ukomeshwe, kwani waathirika na familia zao wanastahili kutendewa haki, ukweli na fidia.”

Ofisi hiyo inasema asilimia kubwa ya mauaji hayo yametokea katika maeneo ya vijijini na kundi linalolengwa Zaidi ni watetezi wa haki za binadamu kwa niaba ya jamii na hususan makundi kama ya watu wa asili na Wacolombia wenye asili ya afrika.

Pia idadi ya wanawake watetezi wa haki za binadamu waliouawa imeongezeka kwa asilimia 50 mwaka 2019 ikilinganishwa na mwaka 2018.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter