Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ofisi ya Miradi ya UN na Benki ya Dunia washirikiana kuboresha maisha ya watu wa Yemen

Watoto wakiwa wamekaa mbele ya nyumba iliyoharibiwa na shambulizi la anga nchini Yemen (Julai 2019)
© UNICEF/Romenzi
Watoto wakiwa wamekaa mbele ya nyumba iliyoharibiwa na shambulizi la anga nchini Yemen (Julai 2019)

Ofisi ya Miradi ya UN na Benki ya Dunia washirikiana kuboresha maisha ya watu wa Yemen

Msaada wa Kibinadamu

Ofisi ya miradi ya Umoja wa Mataifa, UNOPS kwa kushirikiana na Benki ya dunia pamoja na wadau wenyeji, wanafanya juhudi za kuboresha huduma mijini pamoja na nishati ya umeme kwa mamilioni ya watu wa Yemen. Ni kufuatia miaka mitano ya vurugu nchini Yemen ambazo zimeharibu sana miundombinu na huduma za jamii zinazotegemewa sana na watu wa Yemen.

Yemen inakabiliwa na janga kubwa zaidi la kibinadamu duniani. Mgogoro umeweka hatarini usalama na ustawi wa taribani asilimia 80 ya watu wote wa Yemen.

Kwa udhamini wa taasisi tanzu ya Benki ya Dunia, yaani muungano wa maendeleo IDA, UNOPS inafanya kazi na Benki ya dunia kurejesha huduma mijini na pia kuboresha uwezekano wa watu wa vijijini kupata nishati ya umeme.

Moja ya miradi muhimu na bunifu ni kuondoa taka zilizorundikana katika maeneo ili maeneo hayo yapate matumizi mapya.

Zaidi ya tani milioni moja za taka zimekusanywa na kuharibiwa. Na zaidi  ya ajira 650,000 za muda zimetengenezwa na kuwasaidia watu kupata kipato cha kujipatia mahitaji ya msingi. Zaidi ya watu 635,000 hivi sasa wanapata maji safi na salama ya kunywa na huduma za kujisafi ikiwa ni matokeo ya msaada wa pampu, jenereta, paneli za sola katika kituo cha kuzalisha maji.

Kilomita 171 za kuunganisha mitaa na mji zimekarabatiwa. Megawati 11,350 za umeme zimezalishwa kwa ajili ya vituo vya afya, shule, taa za barabarani, na usambazaji wa maji.

Kupitia katika mradi wa umeme wa dharura, mitambo midogo ya nishati ya jua 26,000 imenunuliwa ili kuuzwa kwa bei punguzo kwa familia za vijini. Vituo 342 vya afya, shule, visima vidogo vya maji, vimechaguliwa ili kuunganishiwa mitambo ya kuzalisha umeme kwa nishati ya jua.

Watu wa Yemen milioni mbili, watafaidika kutokana na miradi hii ya uboreshaji hali ya maisha.