Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa atangaza vipaumbele vyake kwa mwaka 2020

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Balozi Tijjani Muhammad-Bande alipokutana na askari wanaoshiriki katika programu za mafunzo ya kijeshi na ulinzi wa amani katika chuo cha kijeshoi cha Khawla bint Al Azwar  cha wanawake huko Abu Dhabi
United Nations
Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Balozi Tijjani Muhammad-Bande alipokutana na askari wanaoshiriki katika programu za mafunzo ya kijeshi na ulinzi wa amani katika chuo cha kijeshoi cha Khawla bint Al Azwar cha wanawake huko Abu Dhabi

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa atangaza vipaumbele vyake kwa mwaka 2020

Masuala ya UM

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Tijjani Muhammad-Bande ambaye alichaguliwa kuchukua wadhifa huo mnamo mwezi Septemba mwaka jana 2019, hii leo jumatatu, awewasilisha kwa nchi wanachama, vipaumbele vyake vya mwaka 2020.

Balozi Bande pia ametaja mipango yake ya miezi michache ijayo hususani maadhimisho ya miaka 75 ya Umoja wa Mataifa na pia muongo wa hatua kwa ajili ya Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs.

“Kama ambavyo nimesema mara nyingi, kipaumbele chetu kwa mkutano wa 74 ni utekelezaji wa majukumu yaliyopo, amani na usalama, kutokomeza umaskini, njaa, kuleta elimu bora, kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na ujumuishaji.” Amesema Balozi Muhammad-Bande.

Kuhusu suala la amani na usalama, Balozi Bande ameipigia chepuo diplomasia hususani katika hali ya sasa ya mvutano mpya kati ya Iran na Marekani akisema, “mgogoro huu hauwezi kutengwa kutengwa na  hali pana katika Mashariki ya Kati. Kwa hivyo ni muhimu kwamba tutafute suluhisho kwa suala la Israeli na Palestina, kama yale yanayowahusu Syria, Yemen, Libya na nyingine.”

Rais huyo wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa amedokeza pia kuwa atakuwa mwenyeji wa tukio la terehe 24 mwezi huu wa Januari katika kuadhimisha kwa mara ya pili siku ya kimataifa ya elimu. Hafla hiyo, “italenga katika kubadilisha mfumo wa elimu kupitia ushirika na kuwapa wadau njia ya kubadilishana na kushirikishana njia bora.” Amesema.

Na kwa upande wa njaa ulimwenguni, Balozi Bande amesema ataandaa hafla mwezi ujao wa Februari kuhusu mada ya ushirikiano wa kusini kusini na ushirika wa pembe tatu katika kuboresha kilimo.

Balozi Bande amesema, “tunaweza kutokomeza njaa na kusausaidia kutokomeza njaa ikiwa tutaongeza ushirikiano katika kuifanya sekta ya kilimo kuwa ya kisasa.”

Rais wa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la  Umoja wa Mataifa Balozi Tijjani Muhammad-Bande akizungumza na waandishi wa habari jijini New  York, Marekani, Septemba 2019
UN /Mark Garten
Rais wa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Balozi Tijjani Muhammad-Bande akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani, Septemba 2019

 

Mkutano kuhusu Bahari na mabadiliko ya tabianchi

Aidha Balozi Bande amerejelea kueleza kuwa mkutano kuhusu masuala ya baharí utafanyika mwaka huu wa 2020 kuanzia tarehe 2 hadi 6 mwezi Juni huko Lisbon, Ureno.

Kuanzia 4-5 Februari, mkutano wa maandalizi utaamua mada za majadiliano na pia kutoa mchango wa mapendekezo ya awali kwa ajili ya azimio litakalopitishwa mwishoni.  

Akieleza kwa kina kuhusu mkutano huo amesema kutokana na umuhimu wa mkutano huo, ni muhimu kutumia fursa na faida za mwendo wa kisiasa ulioanzia katika mkataba wa Paris wa mwaka 2015 na pia mkutano wa hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi uliofanyika mwezi Septemba mwaka jana 2019, ili kusongesha hatua zilizolengwa  katika kuiokoa sayari dunia na hatari ambazo kutochukua hatua kunaweza kusababisha.

“Hii ni kweli, hasa kwa kuzingatia kuwa hatukufikia makubaliano katika masuala muhimu katika mkutano wa 25 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP25 mjini Madrid.” Amesisitiza Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa akiendelea kueleza vipaumbele vyake kwa mwaka huu wa 2020.

Profesa Bande amesema pia kuwa atafanya mazungumzo ya ngazi ya juu kuhusu kudhibiti jangwa, mnamo mwezi Juni 9 kwa kiushirikiana na sekretarieti ya mkataba wa Umoja wa Mataifa wa kudhibiti kuenea kwa jangwa, UNCCD.

Udhibiti wa fedha haramu

Tijjani Muhammad-Bande ameongeza kuwa kwa sasa anafanya kazi na Rais wa Baraza la kiuchumi na kijamii la Umoja wa Mataifa, ECOSOC kuhusu mpango wa uadilifu katika masuala ya fedha. Kwa hivyo amesema anatarajia kuwapatia nchi wanachama msingi wa hatua za mapungufu ya kiuchumi yaliyopo hivi sasa kutokana na mtiririko wa fedha haramu, ufisadi, uatakatishaji fedha na ukwepaji kodi.

Ujumuishaji

Kwa upande wa ujumuishaji kila mmoja, amewataka wajumbe wote kushiriki katika maadhimisho ya miaka 25 ya mwaka wa nne wa kimataifa wa wanawake, miaka 20 ya maadhimisho ya azimio namba 1325 kuhusu wanawake, amani na usalama, pamoja na miaka 10 ya Wanawake wa Umoja wa Mataifa yaani UN Women.

Baraza Kuu pia litaandaa kikao cha ngazi ya juu cha vijana mnamo mwezi Machi tarehe 31 mwaka huu wa 2020 kwa kushirikiana na Rais wa ECOSOC.

"Hakuna shaka kuwa tunahitaji kubuni mkakati wa kukabiliana na tatizo linalowakabili vijana wetu, kama vile ukosefu wa elimu bora, na ukosefu wa ajira.” Amesisitiza Balozi Bande.

Akihitimisha, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa amesema katika kuadhimisha miaka 75 ya Umoja wa Mataifa, anazingatia kwamba maadhimisho haya yanatoa fursa kwa nchi wanachama, “kutathimini miaka ambayo Umoja wa Mataifa umekuwepo na kuamua kuhusu mwelekeo wa kuchukua katika miaka ijayo.”