Jinamizi la tetemeko la 2010 bado linaighubika Haiti-IOM

13 Januari 2020

Shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa IOM linasema miaka 10 baada ya tetemeko baya zaidi kuwahi kukikumba kisiwa cha Haiti idadi kubwa ya watu waliotawanywa wameweza kurejea nyumbani lakini bado jinamizi la tetemko hilo linawaandama.

Kwa mujibu wa IOM tetemeke hilo lililotokea Januari 12 mwaka 2010 lilisababisha athari kubwa na kuathiri watu milioni 3, ikiwemo pia kusambaratisha mioundombinu kama nyumba 105,000, kukatili maisha ya watu zaidi ya laki mbili na kuwalazimisha wengine zaidi ya 208, 000 kukosa makazi.

 

Na hadi kufikia leo Januari 13 mwaka 2020 IOM inasema “watu wengi waliotawanywa wameweza kurejea kwenye maeneo yao ya asili lakini bado kuna wengine 32,788 ambao wanaishi katika makazi 22 ya wakimbizi wa ndani nchini Haiti”. Na watu hao hawako tayari kurejea nyumbani ama kwa sababu ya hali ya maisha katika maeneo hayo walikotoka au kwa sababu hawako tayari kurejea kwa sababu ya kuchelewa kukamilika kwa ujenzo wa nyumba zao.

IOM hata hivyo inasema makadirio yake hayajumuishi hali halishi ya athari na changamoto zinazoendelea kwa mamilioni ya watu kutokana na tetemeko hilo la miaka 10 iliyopita hususan kwa waliotawanywa.

Na kwa ombi la serikali ya Haiti IOM pia haijumuishi idadi ya makambi na makazi yasiyorasmi ambayo yalianzishwa nchi nzima wakati wa dharura na baada ya dharura hivyo idadi za ambao bado wanakabiliwa na changamoto huenda ikawa kubwa zaidi.

IOM imeongeza kuwa majanga mengine ambayo yameendelea kuisakama Haiti baada ya tetemeko la 2020 hadi sasa pia yamechangia hali ya maisha kuzorota ikiwemo kutawanya watu zaidi kama mlipuko wa kipindupindu.

Shirika hilo limetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuendelea kuisaidia Haiti hususan kwa hali inayotia wasiwasi mkubwa ya watu kuendelea kuwa wakimbizi wa ndani ambayo haionyeshi dalili ya kupatiwa suluhu hivi karibuni.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter