Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Leo Januari 12 ni miaka 10 tangu kutokea tetemeko kubwa Haiti:UN

Waokoaji wapekua katika jengo la Umoja wa Mataifa lililoharibiwa na tetemeko la ardhi ambalo liligonga Haiti mnamo 12 Januari, 2010.
UN Photo/Sophia Paris
Waokoaji wapekua katika jengo la Umoja wa Mataifa lililoharibiwa na tetemeko la ardhi ambalo liligonga Haiti mnamo 12 Januari, 2010.

Leo Januari 12 ni miaka 10 tangu kutokea tetemeko kubwa Haiti:UN

Amani na Usalama

Leo Jumapili Januari 12 ni miaka 10 tangu kutokea tetemeko kubwa kabisa kisiwani Haiti ambalo mbali ya uharibifu wa mali lilikatili maelfu ya maisha ya watu.

Katika ujumbe wake maalum kwa ajili ya siku hii Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema siku hii, tunakumbuka mamia ya maelfu ya Wahaiti waliopoteza maisha na mamilioni walioathirika vibaya na tetemeko baya la ardhi lililopiga nchi hiyo miaka kumi iliyopita.

Amemeongeza kuwa “Tunawakumbuka pia wafanyakazi wenzetu mia moja na wawili wa Umoja wa Mataifa waliopoteza maisha siku hiyo. Sitowahi kusahau pigo na huzuni iliyotanda kwenye Umoja wa Mataifa baada ya kutambua ukubwa wa janga hilo. Moyo wangu uko pamoja na wale walipoteza familia, marafiki au wapendwa wao. “

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, Haiti imejijengea mnepo kupitia nguvu za watu wake na msaada wa mafariki zake wengi kuinuka tena kutoka kwenye janga hilo.

Kwa msaada wa jamii ya kimataifa, Haiti inajizatiti kufikia malengo ya maendeleo endelevu, ikiwemo kupitia kuimarisha taasisi ambazo ni muhimu kwa mustakabali na ustawi wa watu wake. Ameongeza Bwana Guterres.

 KKisha akasisitiza “Kwa siku ya leo ninarejelea dhamira ya Umoja wa Mataifa kusaidia Haiti na watu wake kujenga mustakabali bora.”

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa zaidi ya watu laki 2 walipoteza maisha na wengine takriban milioni 3 waliathirika na tetemeko hilo kubwa zaidi kuwahi kukikumba kisiwa cha Haiti na kusambaratisha miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara, vituo vya afya, shule na huduma zingine za msingi.