UNHCR yakaribisha sheria mpya El Salvador kusaidia wakimbizi wa ndani

10 Januari 2020

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi la UNHCR, limekaribisha kupitishwa kwa sheria mpya nchini El Salvador, ya kuwasaidia na kuwalinda wakimbizi.

Sheria hiyo itakuwa mkombozi wa maelfu ya wakimbizi kutoka Amerika ya Kati. Kwa mujibu wa UNHCR sheria hiyo ni ya kuwalinda, na kuwasaidia na inatoa suluhu ya kudumu kwa wakimbizi wa ndani waliotokana na machafuko ya uhalifu wa kupangwa na magenenge ya uhalifu lakini pia wale walio katika hatari ya kutawanywa.

Sheria hiyo iliyopitishwa kwa kura nyingi katika bunge la taifa la El Salvador tarehe 9 mwezi Januari mwaka huu, inafungua milango kwa maelfu ya waathirika wa utawanywaji wa lazima ndani ya nchi, kuweza kupata  misaada ya kibinadamu ya kuokoa maisha na pia kuweza kurejeshewa haki zao za msingi zikiwemo uwezo wa kupata haki za kisheria.

Sheria pia inatoa, kwa mara ya kwanza, mfumo muhimu wa kitaifa ambao unaleta pamoja taasisi mbalimbali tofauti za taifa kushirikiana katika kushughulikia na kuzuia watu kufurushwa makwao.

Ikishatiwa saini na Rais Nayib Bukele, sheria itakuwa na mchango chanya kwa maisha ya raia wa El salvador 71,500 wanaokadiriwa kuwa walifurushwa kati ya mwaka 2006 na 2016 ndani ya mipaka ya nchi yao, na pia maelfu ya wengine zaidi ambao wako katika hatari ya kururushwa katika makazi yao.

Sheria hiyo iliyoandaliwa kwa msaada wa kiufundi kutoka kwa UNHCR, inarandana na kanuni za miongozo ya Umoja wa Mataifa kuhusu wakimbizi wa ndani na viwango vingine vya kimataifa ambavyo vinafafanua haki za wakimbizi wa ndani. Katika nchi ya Honduras ambako inakadiriwa watu 247,000 wamefurushwa makwao, ndani ya nchi yao, bunge linafikiria sheria kama hiyo ambayo imepitishwa na El Salvador.

UNHCR inarejelea ahadi yake ya kuendelea kutoa msaada wa kufundi kwa serikali za America ya kati na Mexico kuwasaidia katika kushughulikia vyanzo na matokeo mabaya ya ufurushwaji wa watu.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud