Machafuko ya kikabila Ituri DRC yaweza kuwa uhalifu dhidi ya ubinadamu:UN

10 Januari 2020

Ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu iliyotolewa leo Ijumaa inasema mauaji, ubakaji na mifumo mingine ya ukatili inayowalenga jamii ya Wahema katika jimbo la Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC inaweza kuwa ni uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na ofisi ya pamoja ya haki za binadamu DRC (UNJHRO), imebainika kwamba angalau watu 701 wameuawa  na wengine 168 kujeruhiwa wakati wa mapigano ya kikabila baina ya jamii za Wahema na Walendu katika maeneo ya Djugu na Mahagi tangu Desemba 2017 hadi Septemba 2019. Ripoti pia imesema watu 142 wamefanyiwa ukatili wa kingono wengi wakiwa ni kutoka jamii ya Wahema.

Rupert Colville ni msemaji wa ofisi ya haki za binadamu Geneva Uswisi

(SAUTI YA RUPERT COLVILLE)

“Tangu Septemba 2018 kundi lililojihami kwa silaha la Lendu limekuwa likijipanga vizuri Zaidi na kufanya mashambulizi dhidi ya Hema na watu wa makundi mengine ya kikabila kama Alur. Miongoni mwa malengo yao ni kudhibiti ardhi ya jamii za Wahema na rasilimali zao. Pia kumekuwa na visa vya kubaka wanawake na watoto wengine wakiwa katika sare za shule kuuawa, uporaji na kuchoma vijiji.”

Ripoti imeongeza kuwatarehe 10 Juni 2019 katika wilaya ya Torges mwanaume wa kabila la Hema aliyekuwa akijaribu kuzuia washambuliaji wenye silaha kumbaka mke wake alishuhudia mwanaye wa miaka 8 akiuawa kwa kukatwa kichwa.

Ripoti imeeleza kwamba “Unyama huu wa hali ya juu wa mashambulizi hayo ikiwemo kukata vichwa wanawake na watoto kwa kutumia mapanga , kuwakatakata viungo vya mwili watu na kunyofoa baadhi ya viungo vyao vya mwili na ngao za Ushindi wa vita vinadhihirisha dhamira ya washambuliaji kutaka kuweka athari isiyosahaulika kwa jamii za wahema na kuwalazimisha kufungasha virago kukimbia na kutorejea tena katika vijiji vyao”

Ripoti inasema machafuko yaliyoorodheshwa yanaweza kuwa na baadhi ya vipengele ambavyo ni uhalifu dhidi ya ubinadamu kupitia mauaji, utesaji, ubakaji na mifumo mingine ya ukatili wa kingono, uporaji na kuteswa.

Pia shule na vituo vya afya vimeshambuliwa  na kusambaratishwa. Kwa mujibu wa ripoti mashambulizi mengi yalifanyika mwezi Juni wakati wa kipindi cha mavuno na Desemba wakati wa msimu wa upanzi. ”Hali hii inafanya kuwa vigumu sana kwa Wahema kulima mashamba yao na kuwaongeza tatizo la ukosefu wa chakula.”

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, tangu Februari 2018 takriban watu 57,000 wamepata hifadhi katika nchi jirani ya Uganda na wengine wengi zaidi ya 556,000 wamekimbilia katika nchi nyingine za jirani. Na makambi mengi ambayo yamekuwa yakihifadhi watu wa kabila la Wahema yamevamiwa, kuchomwa moto na kuharibiwa kabisa na makundi yenye silaha ya Walendu.

Ripoti hiyo imependekeza kwamba malaka ya DRC ishughulikie mizizi ya machafuko hayo  kama vile fursa ya kupata rasilimali ikiwemo ardhi na kuendeleza juhudi za maridhiano baina ya jamii hizo mbili.

Pia imetoa wito wa kuimarisha uwepo wa taasisi za serikali na jeshi katika eneo hilo kuhakikisha usalama wa jamii zote na kuishi kwao wa amani.

Ripoti pia imeitaka mamlaka ya DRc kuendesha uchunguzi huru, usio na upendeleo dhidi ya machafuko hayo na kuhakikisha haki ya kusafirisha waathirika na fursa ya kupata huduma za afya na kisaikolojia inadumishwa.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud