UNICEF kupewa dola milioni 2 na China kusaidia waathirika wa kimbunga Idai Zimbabwe

9 Januari 2020

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF nchini China, limetangaza hii leo kuwa mnamo tarehe 12 mwezi Desemba mwaka jana 2019, lilitia saini makubaliano ya msaada wa dola milioni mbili na Shirika la maendeleo la China, CIDCA ili kuwasaidia watu walioathirika na kimbunga Idai nchini Zimbabwe.

Mchango huo unatoka katika mfuko wa Ushirikiano wa Kusini Kusini wa serikali ya China, SSCAF.

Kimbunga Idai ni janga baya zaidi la asili kusini mwa Afrika katika takribani miongo miwili. Na kimbunga hicho kiliipiga Zimbabwe tarehe 15 mwezi Machi 2019 kikisababisha uharibifu mkubwa wa makazi na maisha na kuwaathiri watu 270,000 wakiwemo watoto 129,600 walioachwa katika mahitaji ya msaada wa kuokoa maisha.

Mwakilishi wa UNICEF nchini China, Cynthia McCaffrey amesema, “mchango wa serikali ya China utaisaidia UNICEF kuweza kusaidia katika dharura nyingine ya kibinadamu. Tutafanya kazi pamoja kufikia watoto walioathirika pamoja na familia zao, tukiwa na maji, vifaa vya kujisafi, afya, lishe na huduma za ulinzi wa jamii.”

Mapema mwaka huu,UNICEF na serikali ya China walishirikiana chini ya mpango wa SSCAF kutoa msaada wa kibinadamu kwa watu walioathirika na kimbunga nchini Msumbuji na Malawi ambako inakadiriwa watu milioni mbili wako katika uhitaji mkubwa wa misaada ya kibinadamu wakiwemo watoto milioni moja.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter