Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yatoa maoni kwa EU kufanya 2020 kuwa mwaka wa mabadiliko kwa ulinzi wa wakimbizi

Muungano wa Ulaya na shirika la  msalaba mwekundu wanasaidia maelfu ya wakimbizi wa Venezuela waliosaka hifadhi maeneo tofauti Amerika ya Kusini. Colombia inawawezesha kupata nyaraka za kuvuka mpaka.
2018 European Union/N. Mazars
Muungano wa Ulaya na shirika la msalaba mwekundu wanasaidia maelfu ya wakimbizi wa Venezuela waliosaka hifadhi maeneo tofauti Amerika ya Kusini. Colombia inawawezesha kupata nyaraka za kuvuka mpaka.

UNHCR yatoa maoni kwa EU kufanya 2020 kuwa mwaka wa mabadiliko kwa ulinzi wa wakimbizi

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, limezindua mapendekezo ya matamanio lakini yanayoweza kufikiwa kwa urahisi kwa mwaka 2020 kwa Croatia na Ujerumani, ambazo ni maraisi wa Baraza la Muungano wa Ulaya,EU. Mapendekezo hayo ni kuhusu ulinzi kwa wakimbizi

Urais na mpango uliokusudiwa wa EU kuhusu uhamiaji na hifadhi, vinatoa fursa za kipekee za kulinda kwa ubora watu waliohaamishwa kwa lazima na pia watu wasio na utaifa barani Ulaya na nje, wakati wanaunga mkono nchi wenyeji.

“Tunapoingia katika muongo mpya, na kufuatia mafanikio ya mkutano wa kimataifa kuhusu wakimbizi, Muungano wa Ulaya chini ya urais wake una nafasi ya kuufanya mwaka 2020 kuwa mwaka wa mabadiliko wa ulinzi mkubwa kwa wakimbizi,” amesema Gonzalo Vargas Llosa, mwakilishi wa kanda wa UNHCR kuhusu masuala ya Muungano wa Ulaya.

Mapendekezo ya UNHCR yanajikita katika mfumo wa hifadhi wa kawaida na unaofaa ndani ya Muungano wa Ulaya EU kupitia mageuzi endelevu na msaada wa kifedha kwa nchi ambazo zinawakaribisha watu waliolazimika kuhama makwao nje ya Muungano wa Ulaya.

UNHCR imesema ndani ya EU, taratibu za haki na za haraka za hifadhi zinahitajika kuanzishwa ili kuamua haraka nani anahitaji kinga ya kimataifa na nani haitaji. Watu wanaostahili ulinzi wanapaswa kupewa hadhi haraka na kupokea msaada kwa ujumuishaji. Wale ambao hawastahili aina yoyote ya ulinzi wanapaswa kusaidiwa katika kurudi kwao.

"Muongo uliopita ulikuwa wa kuhamishwa. Muongo huu unaweza kuwa, na kwakweli unapaswa kuwa moja ya suluhisho, kuanzia sasa katika mwaka 2020,"amesema Vargas Llosa na kuongeza kuwa, “kwa kuunga mkono nchi kubwa zinazohudumia wakimbizi nje ya Ulaya, EU pia inaweza kusaidia wakimbizi kustawi na sio kuishi tu."

Asilimia 85 ya wakimbizi wote duniani wako katika nchi za jirani na wanakotoka na pia katika nchi zinazoendelea, pia msaada wa kifedha unahitajika.