Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa afya wa Benki ya dunia, mkombozi kwa maeneo ya pembezoni-Afghanstan

Mkunga katika kituo cha afya cha Sa-e-Hause kwenye kijiji cha Tajikhan nchini Afghanistan akizungumza na mama aliyembeba mwanae mwenye umri wa miezi 5.
World Bank/Graham Crouch
Mkunga katika kituo cha afya cha Sa-e-Hause kwenye kijiji cha Tajikhan nchini Afghanistan akizungumza na mama aliyembeba mwanae mwenye umri wa miezi 5.

Mradi wa afya wa Benki ya dunia, mkombozi kwa maeneo ya pembezoni-Afghanstan

Afya

Ufadhili wa Benki ya dunia wa kuboresha huduma za karibu za afya katika makazi ya watu wa wilaya iliyoko mbali na mji ya jimbo la Samangan, nchini Afghanistan kumeokoa maisha ya wengi. Kituo cha afya cha Hazrat Sultan sasa kinawaokoa wakazi wa Hazrat na adha ya safari ndefu kufuata huduma za afya. 

Ni maeneo ya mbali na mji, chini ya milima ilipo wilaya ya Hazrat Sultan, kaskazini mwa jimbo la Samangan Afghanstan.

Kituo hiki kinawahudumia wastani wagonjwa 300 kila siku na kina uwezo wa kuwalaza wagonjwa watano.

Ni moja ya vituo 45 katika eneo la Samangan vinavyotoa huduma ya msingi ya afya kupitia mfumo unaofahamika kama SEHAT ukidhaminiwa na Benki ya dunia kwa kushirikiana na serikali ya Afghanstan.

Zarghoona ni mmoja wa wakazi 24,000 wa wilaya ya Hazrat Sultan ambao sasa hawalazimiki kusafiri mwendo mrefu kufuata huduma za kifya.

(Sauti ya Zarghoona)

“Nilikuja hapa, na ninafurahia eneo hili. Nilikuwa na ugonjwa na nilikuja kumwona daktari. Tunapokuwa hapa, wanatupatia dawa na kututibu vizuri, jambo ambalo linanifurahisha. Mazingira ni masafi na madaktari wanafanya uangalizi wa karibu kwa wagonjwa wao”.

Dkt Nesar Ahmad Jawid ni Kaimu Meneja Mradi anasema,

(Sauti ya Dkt Nesar)

"Vituo vinatoa huduma ya afya katika maeneo ambayo takribani watu 2000 hadi 3000 wanaishi. Kuna maendeleo ya wazi kabisa katika hali ya afya ya watu na uelewa wao kuhusu afya umeongezeka".