Nimekasirika, ni watu wachache wanaotaka kuongea kuhusu walibya-Salameh

6 Januari 2020

 

Ghassan Salameh, mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, ameliarifu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Libya kupitia  kikao cha faragha cha mashauriano kilichofanyika jumatatu hii leo katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa Mjini New York.

Akizungumza na wanahabari baada ya mkutano wa Baraza, Bwana Salameh amesema, “hali ni mbaya hivi sasa. Mimi ni wa kwanza kukiri hivyo, lakini wacha pia nisisitize azimio letu kama Umoja wa Mataifa, kujaribu kutafuta njia ya kuondokana na hali hii.”

Aidha amesisitiza kuwa, “hakuna suluhisho la kijeshi nchini Libya.” Na akatoa wito kwa pande zote nchini Libya, “kusimamisha tabia ya mvutano na kuja pamoja ili kukubaliana, makubaliano ya kugawana madaraka ambayo ni sehemu ya suluhisho la msingi la kisiasa.”

Alipoulizwa na wanahabari khusu nchi mbalimbali ambazo zinatangaza kupeleka vikosi vya kijeshi na misaada ya kijeshi ncjhini Libya, Mwakilishi huyo maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema, ujumbe wake uko wazi, “ondokeni Libya.”

Vilevile Bwana Salameh, amesema, “kuna silaha za kutosha nchini Libya hawahitaji silaha zaidi. Kuna wapiganaji mamluki nchini Libya, sitisheni kupeleka mamluki kama ilivyo hivi sasa, mamia, pengine maelfu wanaingia katika Libya hivi sasa.”

Salameh katika hali ya kusononeka amesisitiza, “nimekasirika kuona kila mtu anataka kuongea kuhusu Libya lakini ni watu wachache wanaotaka kuongea kuhusu walibya. Nini kinawakumba walibya? Nini kinawakumba wafanyakazi wahamiaji milioni moja walioko Libya? Ni nini kinawakumba watu hawa? Kwa nini hatuuulizi kuhusu wao? Libya siyo pekee habari ya mafuta? Libya siyo pekee habari ya gesi. Libya siyo pekee Habari ya mifarakano ya mataifa, ni Habari ya binadamu pia. Na watu wanateseka. Na bila sababu nyingine yoyote lakini kwa ukweli kuwa hakuna ujumbe wa wazi wa kimataifa, imetosha.”

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter