Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maroketi matatu yameanguka karibu na kituo cha wakimbizi Libya tunahofia usalama wao:UNHCR

Wakimbizi kutoka Somalia, Syria na Eritrea ambao wameachiwa kutoka vizuizini nchini Libya wakifuata utaratibu wa kuondolewa kutoka kwa kituo cha kuondoka Tripoli, Libya.
© UNHCR/Mohamed Alalem
Wakimbizi kutoka Somalia, Syria na Eritrea ambao wameachiwa kutoka vizuizini nchini Libya wakifuata utaratibu wa kuondolewa kutoka kwa kituo cha kuondoka Tripoli, Libya.

Maroketi matatu yameanguka karibu na kituo cha wakimbizi Libya tunahofia usalama wao:UNHCR

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema linahofia usalama wa mamia ya wakimbizi na waomba hifadhi waliokusanyika katika kituo cha makutano na kuondoka (GDF) kilichopo mjini Tripoli nchini Libya.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na mkuu wa ofisi ya UNHCR nchini Libya Jean-Paul Cavalieri, hofu yao inatokana na taarifa kwamba kuna maroketi matatu yameanguka leo karibu na kituo hicho ingawa kwa bahati nzuri hakuna aliyekufa wala kujeruhiwa.

Kituo hicho kiko chini ya mamlaka ya wizara ya mambo ya ndani ya Libya na UNHCR na mshirika wake LibAid wameruhusiwa na serikali ya Libya kutoa huduma kwenye kituo hicho tangu kilipofunguliwa Desemba 2018.

Kituo hicho cha GDF kilianzishwa kwa lengo la kuhifadhi wakimbizi wanaosubiri kuondoka ambao tayari  wamepatiwa suluhu  ya kupelekwa nje ya Libya.

Kwa mujibu wa UNHCR kituo hicho ambacho kwa sasa kina watu karibu 1000 wakiwemo makundi ya watu karibu 900 walioingia wenyewe tangu Julai mwaka jana, kimefurika na hakifanyi kazi tena kama kituo cha mpito.

UNHCR imezitaka pande zote katika mzozo wa Libya kuwalinda raia na miundombinu yao.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa atoa neno

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake mjini New York Ijumaa jioni amerejelea wito wake wa kusitishwa mara moja mapigano nchini Libya na pande zote husika kurejea kwenye meza ya majadiliano.

“Uungaji mkono wowote kutoka nje kwa makundi yanayopigana, kutaongeza zaidi mgogoro na kuweka ugumu katika juhudi za kufikia amani na suluhisho mjarabu la kisiasa.” Imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Bwana Guterres amerejea pia kusema kuwa kuendelea kukikuka zuio la silaha lililowekwa na Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kupitia azimio namba 1970 ya mwaka 2011 na kama yalivyoboreshwa katika maazimio ya baadaye, kunaifanya hali kuwa mbaya zaidi.