Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuna maeneo 15 yanayohitaji msaada wa dharura 2020:WFP

Mamilioni ya wazimbabwe wanakabiliwa na njaa wakati ukame na janga la kiuchumi vikishuhudiwa.
WFP/Matteo Cosorich
Mamilioni ya wazimbabwe wanakabiliwa na njaa wakati ukame na janga la kiuchumi vikishuhudiwa.

Kuna maeneo 15 yanayohitaji msaada wa dharura 2020:WFP

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP leo limeainisha maeneo 15 ambayo yatahitaji msaada wa dharura na uwekezaji kwa mwaka huu wa 2020. 

Kwa mujibu wa ripoti ya WFP “Maeneo yaliyoa hatarini duniani 2020” Haiti inashikilia nafasi ya kwanza ikielezewa iko katika hatari kubwa ya kutumbukia zaidi katika mgogoro endapo hatua za haraka, msaada na uwekezaji havitopatikana kwa mwaka huu wa 2020. Mmoja wa wakulima wa mbogamboga nchini humo Osena Previlon amenukuliwa na WFP akisema “Hatuishi vuzuri, hatuli vizuri na hatuwezi hata kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa sababu ya zahma iliyoikumba nchi yetu”

Kwa mujibu wa WFP machafuko ya kisiasa na kijamii yameitumbukiza nchi hiyo katika mtafaruku mkubwa huku bei za chakula Haiti zikipanda kwa asilimia 40 na mtu mmoja kati ya watatu nchini humo sawa na watu milioni 3.7 wanahitaji msaada wa haraka wa chakula vijijini na mijini na miongoni mwao milioni 1 wanakabiliwa na janga la njaa.

WFP inaitaka dunia kuwekeza mabilioni ya dola 2020 ili kukomesha hali ya kutokuwa na uhakika wa chakula inayoongezeka kote duniani.

Ripoti hiyo imesema Zimbabwe ni nchi nyingine iliyo katika hatari ambayo imeshuhudia ukame mbaya zaidi mwaka 2019 na utakapowadia msimu wa muambo Februari WFP inasema chakula chote kitakuwa kimeisha na watu milioni 7.7 wanakabiliwa na njaa na kuhitaji msaada wa chakula.

Sudan Kusini kwa mujibu wa ripoti hiyo bado kunatokota kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe watu milioni 3.8 wametawanywa na mafuriko ya 2019 yamewaathiri takriban watu milioni 1 na kuathiri tani Zaidi ya 73,000 za nafaka hali ambayo imewafanya baadhi ya wakulima nchini humo kujiuliza “endapo Mungu amewasahau”

Maeneo mengine yaliyotajwa na ripoti hiyo ni Ukanda wa Sahel, Mali, Burkina Fasso na Magharibi mwa Niger ambako ni kutokana na mchanganyiko wa sababu ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, vita, na mamilioni ya watu kutawanywa.

WFP inakadiria kuwa itahitahi Zaidi ya dola bilioni 10 mwaka huu wa 2020 ili kufadhili operesheni zake katika Zaidi ya nchi 80 kote duniani na bila fedha hizo mipango yote ya uzaidizi itakuwa njiapanda.

WFP imeongeza kuwa “Dunia ni sehemu isiyosameheka na tunapofungua ukurasa mpya 2020, WFP inakabiliwa na changamoto mpya na kubwa zinazohitaji kushughulikiwa kwa haraka ili kuokoa maisha.”