Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa wazindua majadiliano ya maadhimisho ya 75 ya Umoja wa Mataifa

Makao makuu ya UN, New York, Marekani
UN Photo/Cia Pak
Makao makuu ya UN, New York, Marekani

Umoja wa Mataifa wazindua majadiliano ya maadhimisho ya 75 ya Umoja wa Mataifa

Masuala ya UM

Leo tarehe pili mwaka 2020, umeshuhudiwa uzinduzi wa mkakati wa Umoja wa Mataifa wa majadiliano makubwa zaidi ya kimataifa kuhusu mstakabali wa dunia. Ni majadiliano makubwa ya pamoja kuhusu jukumu la ushirikiano wa kimataifa  katika kujenga mstakabali bora kwa wote. Mpango huo utashuhudia Umoja wa Mataifa ukichochea majadiliano katika mwaka huu mpya wote wa 2020 kwenye mazingira tofauti kote duniani. 

Majadiliano ya maadhimisho ya 75 Umoja wa Mataifa, UN75 pamoja na ‘ukaguzi wa dakika moja’ mtu yeyote anaweza kuufanya, kura za maoni katika nchi 50 na pia uchambuzi wa akili bandia  wa vyombo vya habari vya jadi na mitandao ya kijamii katika nchi 70, vitatoa takwimu za kufahamisha sera na mijadala ya  kitaifa na kimataifa.

Katika kutoa wito wa ushiriki, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema, “hakuna nchi, hakuna jumuiya ambayo peke yake inaweza kutatua matatizo magumu ya dunia yetu. Tunahitaji kuungana pamoja, siyo tu kuzungumza, lakini pia kusikiliza. Ni muhimu pia kuwa nyote mshiriki katika mazungumzo. Tunahitaji maoni yenu, mikakati yenu na mawazo ili tuweze kuwahudumia vizuri watu wa ulimwengu ambao tunatakiwa kuwahudumia.”

Ikiwa na lengo la kuhusisha maeneo kadha katika kila mipaka, sekta mbalimbali na vizazi, timu ya UN75 inashirikiana na mtandao wa sekta ikijumuisha waratibu wakazi wa Umoja wa Mataifa, kwa ajili ya ufanikishaji wa kufikisha taarifa kote na majadiliano kufanyika katika kila nchi duniani.

Katika zoezi la usikilizaji la ulimwengu, pamoja msisitizo kwa vijana na makundi ambayo hayajashirikishwa na Umoja wa Mataifa, mkakati wa UN75 unalenga kuelewa matarajio  ya ushirikiano wa kimataifa katika kushinikiza changamoto za ulimwengu.

Maoni na mawazo ambayo yatatolewa, yatawasilishwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa viongozi wa Ulimwengu na maafisa wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa mnamo Septemba 21, 2020, katika hafla ya ngazi ya juu ya kuadhimisha miaka 75 ya Umoja wa Mataifa.

Ili kuhamasisha na kuarifu kuhusu majadiliano haya, Umoja wa Mataifa pia unashiririkiana na Studio ya Vox Creative ili kutengeneza video ya mahojiano ya watu 38 kutoka kote ulimwenguni, wakielezea uzoefu wao na maoni yao kuhusu masuala muhimu ya kidunia. Hiyo itazinduliwa mnamo tarehe 6 ya mwezi huu wa Januari, 2020

Wale ambao wangependa kuwa sehemu ya majadiliano haya, wao wenyewe au kwa njia ya mtandao, wanaweza kufahamu jinsi ya kujiunga kupitia www.un.org/UN75