Nilivutiwa na ndege na nikasema bila shaka nataka kuwa rubani-Mkimbizi Maya Ghazal

1 Januari 2020

Msichana mkimbizi kutoka Damascus Syria ambaye sasa anaishi Uingereza, hivi karibuni alirusha ndege kwa mara ya kwanza akiwa peke yake, ikiwa ni moja ya hatua muhimu katika safari yake ya masomo ambayo yatamfanya kuwa rubani wa kwanza wa kike mkimbizi kutoka Syria. 

Ni Maya akikutana na Dougals Booth, muigizaji nyota mwingereza na balozi wa shirika la Umoja wa Mataifa nla kuhudumia wakimbizi, UNHCR, kabla ya msichana huyo kuirusha ndege peke yake bila kutegemea usimamizi wa walimu wake. Ni siku ambayo msichana huyu mwenye umri wa miaka 20 anaipaisha ndege katika moja ya hatua ya kuelekea kupata leseni ya urubani.

Baba yake Maya alikimbilia Uingereza baada ya vita kuanza, na kisha kupitia mpango amaalumu wa kuziunganisha familia, Maya aliungana na Baba yake na akapata nafasi ya kujiunga na masomo nchini humo Uingereza.

Maya anamwambia Douglas kuwa hali ya hewa inaonekana iko sawa na bila shaka kila kitu kitaenda vyema. Na baada ya maongezi kadhaa kuhusu fursa hasa za kielimu kwa wakimbizi, Maya anasema,“tunataka kutizamwa kama wanadamu wa kawaida, wenye uwezo wa kawaida, na matumaini, ndoto na mstakabali ambao tunataka kuujenga.”

Maya anaeleza kuwa maisha huko Syria baada ya kuanza kwa vita, yalikuwa hayavumiliki. Umeme, maji na hata kwenda shule ilikuwa si salama tena.

Kuhusu alifikiaje uamuzi wa kuwa rubani, Maya anasema, “elimu kwa wakimbizi ni muhimu. Bila elimu, bila watu kutuamini, haitawezekana kwetu kutimiza uwezo na ndoto zetu. Mara zote huwa naangalia ndege na nilivutiwa na na mashine hizo kubwa na nkafikiri hicho ndicho ninachokitaka. Kuwa rubani.”

Maya na Douglas wako tayari kupaa angani kwa ndege ndogo lakini ambayo inaipaisha juu zaidi ndoto yake ya kuwa rubani.

Baada ya muda wanarejea ardhini, na safari imekuwa salama,“leo ni siku yangu ya kwanza ya kupaa peke yangu na ni hatua kubwa kwasababu ni muhimu katika safari yangu ya kuwa rubani wa kwanza mkimbizi kutoka Syria.”

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud