Heri ya mwaka mpya ,nawatakia amani na furaha 2020:Guterres

1 Januari 2020

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo ameungana na dunia kuukaribisha mwaka mpya wa 2020 akiisihi dunia kudumisha amani hasa muongo wa utimizaji wa malengo ya maendeleo endelevu au SDGs ukianza.

Guterres amesema, “tunaingia  mwaka 2020 tukiwa na hali ya sintofahamu na ukosefu wa usalama pande zote duniani. Kuendelea kwa pengo la usawa na ongezeko la chuki na ulimwengu wenye migogoro na sayari yenye ongezeko la joto.”

Amesisitiza kuwa mabadiliko ya tabianchi sio tu tatizo la muda mrefu bali pia ni hatari iliyo bayana na inayoendelea akionya kwamba, “hatuwezi kumudu kuwa kizazi kilichozembea wakati sayari ikiteketea.”

Hata hivyo amesema licha ya changamoto zote hizo lukuki kuna matumaini, mwaka huu, ujumbe wa Mwaka Mpya ni chanzo kikubwa zaidi cha tumaini hilo: vijana wa ulimwengu huu. Kuanzia hatua za mabadiliko ya tabianchi hadi usawa wa kijinsia hadi haki ya kijamii na haki za binadamu, kizazi chako kiko mstari wa mbele na kwenye vichwa vya habari.”

Amesema ametiwa moyo sana na shauku na azma ya vijana katika kuleta mabadiliko na kwamba wako sahihi kudai jukumu katika kuunda mustakabali wa dunia hii. Amewataka vijana kufahamu kwamba yuko pamoja nao, na Umoja wa Mataifa unasimama nao na ni wao.

Mwaka 2020 pia Guterres amesema ni mwaka wa maadhimisho ya miaka 75 ya Umoja wa Mataifa lakini pia, “tunazindua muongo wa hatua kwa ajili ya Malengo ya Maendeleo Endelevu, muongozo wetu kwa utandawazi wenye usawa.”

Amehimiza kuwa mwaka huu, dunia inahitaji vijana kuendelea kupaza sauti, kuendelea kufikiria mambo makubwa, kuendelea kusukuma mipaka, na kuendelea kutoa shinikizo. Ameitakia dunia amani na furaha kwa mwaka 2020.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter