ICC kuchunguza uhalifu wa vita Palestina itakuwa hatua muhimu:UN

31 Disemba 2019

Wataalam wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wamesema itakuwa hatua muhimu kwa mahakama ya kimata ya uhalifu ICC kuchunguza madai ya uhalifu wa vita katika eneo linalokaliwa la Wapalestina itakuwa muhimu sana.

Wataalam hao wamepongeza uamuazi huo wa ICC na kusema ni hatua muhimu katika kuelekea lengo la uwajibikaji kwenye miongo mitano ya ukaliaji wa Israel katika eneo hilo.” Uwajibikaji ulikosekana hadi sasa katika ukaliaji wa miaka 52 ya eneo la Wapalestina” amesema Michael Lynk mwakilishi maalum kuhusu hali ya haki za binadamu katika eneo linalokaliwa la Palestina tangu mwaka 1967.

Ameongeza kuwa “kwa miaka mingi jumuiya ya kimataifa imepitisha mamia ya maazimio kupitia Umoja wa Mataifa kulaani hatua mbalimbali za ukaliaji wa Israel katika eneo la Wapalestina. Lakini ni mara chache kulijumuisha ukosoaji wenye athari kwa Israel, lakini sasa uwezekano wa uwajibikaji hatimaye uko tayari.”

Mwenesha mashitaka wa ICC Fatou Bensouda alitangaza Desemba 20 mwaka huu kwamba “Nimeridhika kwamba ni suala la msingi kuendelea na uchunguzi kuhusu hali ya Palestina”. Bi. Bensouda ametumia miaka mitano kutathjimini  ushahidi wa awali kama sehemu ya awali ya uchunguzi wa mita vya mwaka 2014 Gaza, makazi ya Israel na hivi karibuni kabisa mauaji na kujeruhiwa kwa waandamanaji wa Palestina karibi na mpaka wa Gaza.

Bensouda amesema kwamba kabla ya uchunguzi rasmi kuanzishwa na ofisi yake atauliza uamuzi wa mapema wa kitengo cha kesi kuhusu suala la mamlaka ya ardhi. Hasa, anatafuta uthibitisho kwamba eneo ambalo Mahakama inaweza kutumia mamlaka yake linajumuisha Ukingo wa Magharibi, pamoja na Yerusalemu ya Mashariki, na Gaza.

“Katika ulimwengu unaotangaza kujikita katika haki za binadamu na sheria kwa misingi ya utulivu wa kimataifa, ni muhimu kwa jamii ya kimataifa kutetea uamuzi wa Mwendesha Mashtaka wa ICC ili kuendeleza uchunguzi wake na kutafuta uamuzi mzuri kutoka kwa kitengo cha kesi kuhusu suala la mamlaka ya eneo, "alisema mwakilishi huyo maalum wa haki za binadamu Lynk.

Pia ameongeza kuwa "Sheria za kimataifa lazima ziwe msingi wa kutafuta haki kwa waathirika wa uhalifu wa kivita katika mzozo huu, na jamii ya kimataifa lazima iunge mkono kwa dhati sheria na taasisi ambazo imeziunda na kuzikuza.”

Mwakilishi huyo Maalum alibaini kuwa mwendesha mashtaka pia alikusudia kuchunguza ikiwa wajumbe wa Hamas na vikundi vingine vya Wapalestina wamefanya uhalifu wa kivita katika kipindi hicho tangu Juni 2014. "Ikiwa ushahidi uliokusanywa na mwendesha mashtaka wa ICC unamuongoza kupata matokeo dhidi ya mashirika haya basi juhudi zake lazima pia ziungwe mkono”, amesema mtalaam huyo. "Mkataba wa Roma unamaanisha kutumiwa bila huruma; kwa kweli, hii ndio njia pekee ya kujenga umuhimu wa lazima wa kisiasa na umaarufu wa lengo lake "

Akishughulikia wasiwasi wa muda mrefu kuhusu jinsi magurudumu ya haki yyanavyokwenda polepole katika suala hili, mtaalam huyo maalum ya ametoa wito kwamba suala la mamlaka ya ardhi liwasilishwe na kutatuliwa kwa haraka iwezekanavyo na ikiwezekana na kitengo cha kesi.

"Haki iliyocheleweshwa ni haki iliyokataliwa. Iwapo tuhuma za uhalifu wa kivita zinaendelea katika hatua rasmi ya uchunguzi, kila juhudi inapaswa kufanywa ili kuendeleza kazi ya ofisi ya mwendesha mashtaka kwa haraka haraka sanjari na usawa wa kisheria, ili waathirika wengi wa mzozo huu waweze kutumaini kuwa haki inawezekana kupatikana katika maisha yao. "

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter