Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto zaidi ya 390,000 wamezaliwa leo kote duniani:UNICEF

Kwa mujibu wa UNICEF, watoto zaidi ya 390,000 wamezaliwa leo kote duniani 1 Januari 2020
UNICEF/Ilvy Njiokiktjien
Kwa mujibu wa UNICEF, watoto zaidi ya 390,000 wamezaliwa leo kote duniani 1 Januari 2020

Watoto zaidi ya 390,000 wamezaliwa leo kote duniani:UNICEF

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF leo Januari Mosi mwaka mpya ukisherehekewa kote duniani limetoa wito kwa viongozi wa dunia kuwekeza katika wahudumu wa afya kitaaluma na vifaa ili kuhakikisha wanaokoa maisha ya kila mtoto anayezaliwa. 

Sauti hiyo inaashiria kuna uhai, mtoto amezaliwa. Na ujumbe huo wa UNICEF umekuja wakati leo hii takriban watoto 392,000 wamezaliwa kote duniani.

Kwa mujibu wa mkurugenzi mtendahi wa UNICEF Henrietta Fore, “mwanzo wa mwaka mpya na muongo mpya ni fursa ya kutafakari matumaini yetu na matarajio, sio tu kwa mustakabali wetu bali kwa mustakabali wa wale watakaokuja baada yetu. Wakati kalenda ikibadilika kila Januari tunakumbushwa majukumu yetu sote na uwezekano wa kila mtoto kuanza safari yake ya maisha endapo atapewa fursa.”

Fiji katika ukanda wa Pasifiki ndiko alikozaliwa mtoto wa kwanza wa mwaka mpya wa 2020, na Marekani ni wa mwisho kwa siku hii ya kwanza ya mwaka huu.

Kimataifa zaidi ya nusu ya watoto wote hao 392,000 wamekadiriwa kuzaliwa katika nchi 8 za dunia. Nafasi ya kwanza kwa idadi kubwa ya Watoto waliozaliwa leo  inashikwa na India ambako watoto 76,385 wamezaliwa ikifuatiwa na China zaidi ya Watoto 46,000, Nigeria zaidi ya 26,000, Pakistan zaidi ya 16,000, Indonesia zaidi ya 13,000 , Marekani zaidi ya 10,000 , Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC zaidi ya 10,000 na Ethiopia zaidi ya 8,000.

Kwa upande wa Afrika ya Mashariki Tanzania ndio imeongoza kwa watoto zaidi ya 5,000 ikifuatiwa na Uganda, Kenya, Burundi, Rwanda na Sudan Kusini ya mwisho walikozaliwa watoto 920.

Kila Januari UNICEF husherehekea watoto waliozaliwa siku ya mwaka mpya ambayo ni siku mashuhuri ya watoto kuzaliwa kote duniani. Hata hivyo shirika hilo linasema kwa mamilioni ya watoto wanaozaliwa kote duniani , siku yao ya kuzaliwa si ya faraja kubwa.

Kwani mwaka 2018 watoto wachanga milioni 2.5 walifariki dunia katika mwezi wa kwanza wa maisha yao na karibu theluthi moja kati yao walikufa katika siku ya kwanza ya maisha yao.

Wengi wa watoto hao walikufa kutokana na maradhi yanayoweza kuzuilika kama kuzaliwa njiti, matatizo wakati wa kujifungua na maambukizi.

Mbali ya hayo zaidi ya watoto milioni 2.5 kila mwaka huzaliwa wakiwa tayari wamekufa.

Bi. Fore amesisitiza kwamba, “kina mama wengi na watoto wachanga hawahudumiwi na wakunga na wauguzi waliobobea katika kazi , wenye taaluma ya kutosha na vifaa vinavyohitajika na matokeo yake ni mabaya sana. Tunahitaji kuhakikisha kwamba mamilioni ya watoto wanaishi siku ya kwanza ya maisha yao na kuishi katika muongo huu na zaidi endapo kila mmoja wao atazaliwa katika mikono salama ya wauguzi na wakunga.”