UNAMID yakaribisha muafaka baina ya serikali ya Sudan na Darfur Track

30 Disemba 2019

Mpango wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika AU kulinda amani Darfur Sudan UNAMID, leo umekaribisha mpango wa makubaliano uliotowasaini baina ya serikali ya mpito ya Sudan na kundi la vuguvugu lenye silaha la Darfur liitwalo Darfur Track.

Muafaka huo ulitiwa saini wakati wa mazungumzo ya amani yaliyofanyika Juba Sudan kusini mnamo tarehe 28 Desemba 2019.

Kwa mujibu wa UNAMID muafaka huo unadhihirisha hakua katika mchakato wa amani kwani inaainisha masuala na taratibu muhimu ambazo zitakuwa muongozo katika majadiliano yanayoendelea na kutumika kama msingo kwa ajili ya makubaliano ya amani ambayo yatakuwa na usawa na ya kina.

Mwakilishi wa pamoja wa UNAMID na mpatanishi mkuu Jeremiah Mamabolo, amepongeza utiwaji saini wa mkakati huo wa makubaliano na kusema “Hii ni hatua chanya inayothibitisha utashi wa kisiasa na dhamira ya pande zote katika kufikia makubaliano ya kina ya amani. Tunaipongeza serikali ya mpito ya Sudan nan a pande za Darfur  kwa hatua hii na kuzichagiza kuendelea na uzi huohuo.”

Mamabolo ameongeza kuwa “UNAMID itaendelea kusaidia majadiliano ya amani Juba kwa kuzingatia azio nambari 2495 (2019) la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na ndani ya uwezo wake ili kusaidia pande zote katika mchakato wa majadiliano ili hatimaye kufikia lengo kuu la amani ya kudumu na mustakabali bora kwa watu wote wa Sudan.”

UNAMID imekuwa ikitoa msaada wa kiufundi kwa pande zote za Sudan zinazoshiriki majadiliano ya amani Juba tangu tarehe 10 Desemba 2019 .

Azimio hilo la Baraza la Usalama liliipa jukumu UNAMID kutoa msaada muhimu unaohitajika kwa serikali ya mpito ya Sudan na makundi yenye silaha yanayoshiriki majadiliano hayo ili kusongesha mbele mchakato wa amani.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter