Zaidi ya watoto 170,000 walishambuliwa tangu 2010 katika nchi zilizo na mizozo:UNICEF

30 Disemba 2019

Watoto wanazidi kubeba gharama na kukumbwa na madhila wakati mizozo ikiendelea kushuhudiwa duniani, kwa mujibu wa ripoti ya shirika la kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa , UNICEF iliyotolewa leo. 

Ripoti hiyo inasema tangu mwanzo wa muongo huu, Umoja wa Mataifa umethibitisha zaidi ya visa 170,000 vya ukiukaji mbaya wa haki za watoto sawa na zaidi ya visa 45 vinavyotokea kila siku kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Idadi ya nchi zinazokumbwa na mizozo ni ya juu zaidi tangu kutiwa saini mkataba wa haki za watoto mwaka 1989, huku mizozo hiyo ikikatili maisha ya watoto hao na kuwalazimisha kuhama makwao.

Mwaka 2018 Umoja wa Mataifa ulithibitisha zaidi ya visa 24,000 vya ukiukaji wa haki za watoto ikiwemo mauaji, dhuluma  za kingono, utekaji, kukosa huduma za msingi za binadamu, kuwaajiri watoto jeshini na mashambulizi hospitalini na shuleni.

UNICEF inasema wakati jitihada za kuripoti visa hivi zikiongezeka, idadi nayo inaongezeka, hii ikiwa ni mara mbili, zaidi ya ile iliyorekodiwa mwaka 2010.

Mkurugenzi mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore amesema, “vita vinavyoshuhudiwa kote duniani hivi sasa vinadumu kwa muda mrefu zaidi na kusababisha umwagaji damu mkubwa huku vikikatili maisha ya maelfu ya watoto na barubaru. Mashambulizi dhidi ya watoto yanaendelea bila kukoma wakati pande kinzani zikikiuka moja ya sheria za msingi kabisa za vita, kuwalinda watoto. Ingawa kila kitendo cha ukatili dhidi ya watoto kinachogonga vichwa vya habari kusababisha wito wa kulaani na kutaka hatua zichukuliewe, lakini bado kuna watoto wengi ambao hawalindwi.

Zaidi ya watoto 12,000 waliuawa au kulemazwa mwaka 2018. Kundelea kwa mashambulizi ya angani na kutumiwa silaha zinazolipuka kama mabomu na maroketi, husababisha maafa mengi zaidi miongoni mwa watoto wakati wa mizozo.

UNICEF inatoa wito kwa pande zinazozana kuheshimu sheria za kimataifa na mara moja kumaliza ukiukaji wa haki za watoto na kulenga maeneo ya raia zikiwemo shule, hospitali na miundo msingi ya maji. Pia kwa nchi zilizo na ushawishi dhidi ya zile zilizo na mizozo imezitaka kutumia ushawishi wao kuwalinda watoto.

Kwenye nchi hizo zote, UNICEF inafanya kazi na washirika kuwalinda watoto walio katika hatari kubwa na kuwapa huduma za afya, lishe, elimu na huduma za kuwalinda watoto.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter