Mafunzo ya ufundi ya MINUSCA yametukomboa:Raia wa CAR

24 Disemba 2019

Mafunzo ya ufundi yaliyoanzishwa na Baraza la mashauriano na ubunifu mjini Bangui nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR kwa kushirikiana na mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo MINUSCA yameleta neema kwa raia wa nchi hiyo. 

Mafunzo ya ushonaji ambayo kwa sasa yanahusisha watu 30 ni sehemu ya mradi wa kupunguza machafuko katika jamii na kuwawezesha wanufaika hususani wasiojiweza kuwa na shughuli za kiuchumi. Adepphe Bimba ni mkutugenzi wa baraza hilo

“Kama sehemu ya ushirikiano na ofisi ya Umoja wa Mataifa inabidi tuwape mafunzo wanaufaika ya ujuzi wa msingi wa ushonaji kwa miezi mitatu na miezi mwiwli kuwafundisha jinsi gani ya kufanyakazi kwa ushirikiano au makundi. Na vipindi vya mradi huu vinajikita robo tatu ya muda katika ushonaji na robo iliyosalia ni mafunzo ya upatanishi wa kijamii, utangamano na kudhibiti migogoro. Sio tu tunataka kuwafundisha katika ushonaji bali pia kuwapa msingi wa kuwa viongozi na wapatanishi katika jamii zao.”

Mafunzo haya yanatolewa na wataalam wa mitindo na yanawaleta pamoja katika mazingira rafiki watu kutoja jamii zote. Pia ni njia ya kuchangia kuimarisha jamii zao.

Miongoni mwa washiriki wafaidika ni Nanette Gamanda anayehisi amepewa fursa ya pili katika maisha“Nilikuwa chuoni, sikumaliza shahada yangu kwa sababu ya vita iliyozuka nchini .”

Kwa mujibu wa MINUSCA mafunzo hayo ya ushoni kwa hakika ni shughuli muhimu, inayotambulika kama njia bora ya kuingiza kipato cha haraka kama anavyothibitisha Idriss Zamzam mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo“Nilichagua shughuli hii ili kuwa mfano kwa kaka zangu na kuwaambia kwamba ushonaji sio kwa ajili ya wanawake pkee, ni kazi ambayo hata wanaume wanaweza kuifanya pia.”

Mjini Bangui jumla ya watu 808 wakiwemo wanawake 190 wamefaidika na mafunzo haya, sio tu ya kushona bali pia katika nyanja nyingine kama vile ufundi makenika, biashara, upishi, ufunsi umeme na udereva.

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud