Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ni tete kwa ufadhili wa wakimbizi Uganda-UNHCR

Wakimbizi wakiwa katika kituo cha afya kilichoko katika kambi yao ya Nakivale nchini Uganda
IRIN/Samuel Okiror
Wakimbizi wakiwa katika kituo cha afya kilichoko katika kambi yao ya Nakivale nchini Uganda

Hali ni tete kwa ufadhili wa wakimbizi Uganda-UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limeonya kwamba ufadhili kwa ajili ya msaada kwa wakimbizi nchini Uganda ni mdogo sana.

Uganda inahifadhi jumla ya waomba hifadhi na wakimbizi milioni 1.3 wakiwemo laki moja waliowasili mwaka huu kutoka nchini Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC.

Licha ya idadi hiyo kubwa ya watu wanaohitaji msaada shirika hilo la wakimbizi limesema ufadhili wa fedha uliopatikana ni kidopgo sana ambapo ombi la msaada kwa ajili ya watu hao likiwa limefadhiliwa asilimia 41 tu hadi sasa.

Taarifa ya pamoja iliyotolewa juma hili na mashirika 40 yasiyo ya kiserikali yanayotoa msaada nchini humo imeonya kwamba huduma za msingi inazozitoa kama elimu, huduma za afya, ulinzi na malazi kwa wakimbizi na jamii zinazowahifadhi zinakabiliwa na hatihati ya kufungwa kuanzia mwezi Januari 2020 endapo msaada wa haraka wa fedha za ufadhili hautopatikana.

Kwa upande wake shirika la kimataifa la Save the Children limesema ukosefu wa fedha tayari unaathiri uwezo wa shirika hilo kufikisha huduma za msingi , huku shirika baraza la wakimbizi la Norway likisema baadhi ya wakimbizi wameshaanza kuingia kwenye madeni na wengine kulazimika kupunguza idadi ya milo ili kuhifadhi chakula kingine wakihofia ukata.

Akizungumza jumanne kwenye kongamano la kimataifa la wakimbizi mjini Geneva Uswis waziri wa Uganda kwa ajili ya misaada, maandalizi ya majanga na wakimbizi Hilary Obaloker Onek ameahidi licha ya changamoto zote hizi nchi yake itaendelea kutekeleza sera yake kuhusu wakimbizi na kufungua mipaka yake.