Visa vya kipindupindu vimepungua kwa asilimia 60 duniani:WHO

Mkazi wa Khartoum nchini Sudan akipatiwa chanjo dhidi ya kipindupindu na hii inafanyika kwa msaada wa shirika la afya ulimwenguni, WHO
WHO Sudan
Mkazi wa Khartoum nchini Sudan akipatiwa chanjo dhidi ya kipindupindu na hii inafanyika kwa msaada wa shirika la afya ulimwenguni, WHO

Visa vya kipindupindu vimepungua kwa asilimia 60 duniani:WHO

Afya

Shirika la afya ulimwenguni leo limetangaza habari njema ya kupungua kwa visa vya kipindupindu duniani kote kwa asilimia 60 mwaka 2018. 

Kwa mujibu wa tangazo hilo lililoko kwenye ripoti ya WHO , mafanikio hayo yametokana na mwenendo wa kutia matumaini katika hatua za kuzuia na kudhibiti ugonjwa wa kipindupindu katika maeneo ambayo huathirika sana duniani ikiwemo Haiti, Somalia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC. Akifafanua zaidi kuhusu mafanikio hayo mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema kupungua huku kwa visa kunakoshuhudiwa katika nchi ambazo ni kama kitovu cha mlipuko wa kipindupindu kunaonyesha ongezeko la nchi kujihusisha katika juhudi za kimataifa za kupunguza kasi ya maambukizi na kuzuia milipuko mingine lakini pia inadhihirisha umuhimu wa kampeni za chanjo .”

Hata hivyo mkuu huyo wa WHO amesema wanaendelea kuhimiza kwamba suluhu ya muda mrefu kwa ajili ya kutokomeza kipindupindu iko katika kuongeza fursa za upatikanaji wa maji safi ya kunywa na kutoa huduma muhimu za usafi.

Ripoti inasema kulikuwa na visa vya kipindupindu karibu laki 5  na vifo 2,990 mwaka 2018 katika nchi 34. Mkuu wa program ya kukabiliana na kipindupindu katika shirika la WHO Dkt.Dominique Legros amesema “Tunachokishuhudia cha kupungua kwa idadi ya visa pia mbali ya kampeni kubwa ya chanjo ni nchi nyingi kuanza kuridhia mkakati wa 2030 wa kukomesha kipindupindu katika mipango yao ya taifa. Ni lazima kuendelea kuimarisha juhudi zetu na kuhusisha nchi zote ambazo hukubwa sana na mlipuko wa ugonjwa huo katika makakati wa kimataifa wa kutokomeza kipindupindu.

Karibu dozi milioni 18 za chanjo ya kipindupindu zilipelekwa katika nchi 11 mwaka jana kwa msaada wa muungano wa chanjo ulimwenguni GAVI.

WHO inakadiria kwamba kila mwaka kipindupindu huathiri watu milioni 1 hadi milioni 4 na hukatili maisha ya watu hadi 143,000.