Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMISS inawasaidia watahiniwa kufika katika vyumba vyao vya mtihani Sudan Kusini

Luteni Kanali Richmark Fernandes (wa pili kutoka kulia), mlinda amani kutoka India anayehudumu katika UNMISS nchini Sudan Kusini kama daktari wa wanyama katika eneo la Bor
UNMISS
Luteni Kanali Richmark Fernandes (wa pili kutoka kulia), mlinda amani kutoka India anayehudumu katika UNMISS nchini Sudan Kusini kama daktari wa wanyama katika eneo la Bor

UNMISS inawasaidia watahiniwa kufika katika vyumba vyao vya mtihani Sudan Kusini

Amani na Usalama

Wanafunzi kote nchini Sudan Kusini wakiwemo wale wanaoishi katika vituo vya Umoja wa Usalama vya kuwahakikishia raia usalama, wanafanya mitihani ya mwisho wa mwaka ambapo mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS inafanya kazi ya kuwapeleka wanafunzi wa kambini katika shule wanakofanyia mitihani na pia kuwarejesha.

Video ya takribani dakika mbili na nusu iliyoandaliwa na UNMISS inaanza ikionesha wanafunzi wakikusanyika alfajiri katika kituo cha ulinzi wa raia cha Umoja wa Mataifa mjini Juba wakijiandaa na siku ndefu mbele yao wanapofanya mtihani wao wa mwisho wa mwaka.

Kufanya mitihani ya majaribio ni suala ambalo ni gumu kwa kila mwabnafunzi, lakini ni gumu zaidi kwa vijana hawa barubaru wa Sudan Kusini ambao wamekuwa wakiishi katika kambi tangu vita ya wenyewe kwa wenyewe vilipoanza miaka sita iliyopita.

Wanatakiwa kufanya mitihani yao katika shule ambazo zimeidhinishwa na serikali, jambo ambalo ni changamoto kwa UNMISS ambayo inatakiwa kuwasafirisha wanafunzi 1,250 kama kundi moja.

Rebecca Chol ni mwanafunzi anayreshiriki mtihani wa mwaka huu,“unajua katika kambi za ulinzi wa raia kuna mambo mengi ambayo yanatukabili kama vile mazingira ambayo tunayoishi si mazuri kabisa. Sawa tuna huduma ya maktaba lakini hii haitutoshi. Hivi ndivyo ninavyoona katika kambi. Pengine nje kunaweza kuwa vizuri. Pengine inaweza inaweza kuwa vizuri lakini katika kambi ni vigumu kwasababu tunaishi katika hizo kambi.”

Pamoja na changamoto, wanafunzi wamejiandaa kufanya kila linalowezekana kupata sifa wanazozihitaji ili kutafuta kazi au kundelea na masomo katika Chuo Kikuu.

Familia ya mwanafunzi Samuel Gadet wakiwemo kaka zake wanne na dada zake watatu, wanaishi katika kambi ya ulinzi wa raia katika eneo la Bor, mkoa wa Jonglei Sudan Kusini. Lakini yeye anaishi na kaka yake katika kambi mjini Juba kwasababu ni rahisi kwake kupata elimu. Pamoja na kutengana kwao, familia yake inajitahidi kumsaidia, anasema"changamoto ninazokabiliana nazo katika kambi naweza kusema ni chamoto zaidi lakini nina namna ya kukabiliana nazo kwasababu familia yangu yote wako huko Bor na hivyo wananitumia chochote ninapohitaji ada ya shule na mengine, kwa hivyo wananisaidia.”

Utiwaji saini wa mkataba wa amani mwaka jana, umeboresha hali ya usalama. Zaidi ya watu 645,000 ambao wanaishi katika kambi za wakimbizi na kambi nyingine za wakimbizi wa ndani wamerejea katika makazi yao. Wengi wa wale wanaoishi katika vituo vya Umoja wa Mataifa wanaweza kwa usalama kwenda shuleni, kazini na dukani katika masoko yaliyoko nje ya kambi.