Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi ya wanaume wanaotumia bidhaa za tumbaku imepungua- Ripoti, WHO

Uvutaji wa sigara bara la Asia.
World Bank/Curt Carnemark
Uvutaji wa sigara bara la Asia.

Idadi ya wanaume wanaotumia bidhaa za tumbaku imepungua- Ripoti, WHO

Afya

Shirika la afya ulimwenguni, WHO linakadiria kwa mara ya kwanza kwamba idadi ya wanaume wanaotumia tumbaku imepungua ikiashiria mabadliko katika janga la tumbaku kimataifa. 

Makadirio hayo  yamo kwenye ripoti mpya ya WHO inayoonesha kwamba hatua za serikali zinaweza kulinda jamii dhidi ya tumbaku, kuokoa maisha na kuepusha watu kutoka kwa madhara ya tumbaku.

Katika takriban miongo miwili, matumizi ya tumbaku kimataifa yamepungua kutoka watu bilioni 1.397 mwaka 2000 hadi watu bilioni 1.337 mwaka 2018 kwa mujibu wa ripoti hiyo ya WHO kuhusu mwelekeo wa matumizi ya tumbaku mwaka 2000 hadi 2025 toleo la tatu.

Akizungumza na waandishi wa habari Dkt. Ruediger Krech, ambaye ni Mkurugenzi wa kitengo cha uchagizaji wa afya kwenye WHO amesema katika hatua njema idadi ya wanaume wanaotumia bidhaa za tumbaku inakadiriwa kuwa imepungua kwa watu milioni 2 ifikapo mwaka 2020 hatua ambayo ametaja kuwa muhimu kwani..“Idadi ndogo ya wanaume wanaotumia bidhaa za tumbaku inamaanisha ni watu wachache watakabiliwa na machungu na maafa yatokanayo na matumizi hayo. Kupungua kwa matumizi ya tumbaku kunaashiria kwamba juhudi za kudhibiti matumizi ya tumbaku zimezaa matunda kwa mfano kutoza ushuru, kupiga marufuku uvutaji sigara maeneo ya umma, kuzuia matangazo na kulinda watoto dhidi ya tumbaku.”

Ameongeza kwamba hatua hiyo inatoa matumaini ya kufikia malengo ya kupunguza kwa asilimia 30 matumizi ya tumbaku ifikapo mwaka 2025. 

Hata hivyo ameonya dhidi ya kubweteka.“Hatuwezi kuridhiswa na kupungua kwa idadi wakatu huu ambapo takriban watu bilioni moja wanatumia bidhaa za tumbaku, ni lazima tuimarishe juhudi dhidi ya matumizi ya tubaku kwa ajili ya kulinda kizazi hiki na kijacho bado watu milioni 8 wanakufa kila mwaka kutokana na matumizi ya tumbaku. Kuendela kupunugza matumizi ya tumbaku kutasaidia katika kuokoa maisha, kulea familia na kuimarisha jamii.”

Kwa  mujibu wa WHO, kati  ya vifo hivyo milioni 8, zaidi ya vifo milioni 7 ni kutoka matumizi ya moja kwa moja ya tumbaku huku vifo takriban milioni 1.2 ni kutokana na mtu kuwepo katika mazingira ya wavuta sigara. 

Aidha vifo vingi vitokanavyo na matumizi hayo ya tumbaku vinataokea katika nchi za kipato cha chini na wastani ambako kunashuhudiwa uingiliaji wa viwanda na biashara ya tumbaku.

Ripoti pia inaonesha kwamba watoto milioni 43 wa kati ya umri wa miaka 13-15 walitumia bidhaa za tumbaku mkwa 2018, wanawake milioni 244 walitumia bidhaa hizo mwaka jana.