Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lugha za asili bado ni muhimu kwa mustakabali wa ulimwengu-Bande

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Balozi Tijjani Muhammad-Bande na Liu Zhenmin, msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya uchumi na jamii, wakiwa na washiriki wa tukio la kuhitimishwa kwa mwaka wa kimataifa wa lugha za asili mjini
UN Photo/Rick Bajornas)
Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Balozi Tijjani Muhammad-Bande na Liu Zhenmin, msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya uchumi na jamii, wakiwa na washiriki wa tukio la kuhitimishwa kwa mwaka wa kimataifa wa lugha za asili mjini

Lugha za asili bado ni muhimu kwa mustakabali wa ulimwengu-Bande

Utamaduni na Elimu

Lugha za asili bado ni muhimu kwa mustakabali wa ulimwengu hivyo tufanye kila namna kuzitunza, ni moja ya kauli alizozitoa rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Tijjani Muhammad Bande katika  mkutano wa ngazi za juu wa kuhitimisha mwaka wa kimataifa wa lugha za asili uliofanyika hii leo katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani.

Profesa Bande amesema, “wengine wanaweza kuuliza ni kwa nini kutoweka kwa lugha za asili, watu wa asili au utamaduni wa asili wa maeneo ya mbali vinatakiwa kuwa suala nyeti la umuhimu. Wengine wanaweza kuuliza kuna umuhimu gani kwa binadamu ikiwa aina fulani ya maisha itatoweka na kwa nini Umoja wa Mataifa uyape hayo kipaumbelea!.”

Kisha Profesa Bande akaeleza kwa nini ulimwengu unapaswa kuona kuna umuhimu wa kuyatunza hayo, ikiwemo lugha za asili na watu wa asili, “kwanza lugha ya asili inachangia sana katika kuwafanya watu kufikiria juu ya nafasi yake katika ulimwengu na hususani namna ambavyo taswira hii ya dunia inaweza kuendelezwa na kusisitizwa na kutafuta suluhisho la matatizo makubwa.”

Aidha Balozi Bande amewakumbusha wahudhuriaji kuhusu jinsi utamaduni wa asili ambavyo umesaidia kama njia ya kutumainiwa katika kupitisha na kupata maarifa kutoka kizazi hadi kizazi, “hii ni kama vile maarifa kuhusu dawa za mitishamba, utengenezaji wa vifaa, kuchakata vyakula na kuvihifadhi, utawala wa jamii na serikali pamoja na utatuzi wa migogoro. Dawa za kisasa ni mara chache zinaweza kutengenezwa pasipo kutumia mafanikio ya siku za nyuma.”

Vile vile amesema kutoweka kwa lugha za asili kunawafanya watumiaji wa lugha hiyo kupoteza utambulisho wao.

Wamaasai ni moja ya makabila yanayoishi kiasili
UNDP
Wamaasai ni moja ya makabila yanayoishi kiasili

 

Hata hivyo kuna juhudi zinafanyika

Mojawapo ya juhudi ambazo zimefanyika ni pamoja na uundwaji wa Jukwaa la kudumu la watu wa asili. Pia Umoja wa Mataifa umekuwa chombo kikuu cha kukuza ufahamu kuhusu lugha za asili, na pia hatua zinazotakiwa kuchukuliwa ili kuzuia kutoweka kwa kwake.

“Tukirejea kuanzia mwaka 1982, Umoja wa Mataifa ulianzisha kundi kazi kuhusu watu wa jamii ya asili. Pia mwaka wa kimataifa wa 2019 wa lugha za asili ni ushahidi tosha wa uwajibikaji wa Umoja wa Mataifa katika kuhifadhi lugha zilizoko hatarini.” Amesema Balozi Bande.

Takwimu zinasemaje?

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, kila wiki mbili, takribani lugha moja ya asili inatoweka na hivyo kufaanya takribani lugha mbili za asili kutoweka kila mwezi.

Lugha za asili 4,000 zilizosalia zinazungumzwa  na aasilimia 6 tu ya watu wote duniani.

Ushauri

Balozi Bande ameeleza kuwa ana matumaini hali itakuwa sawa ikiwa taasisi za kielimu, sekta binafsi na wadau wa jamii awatachukua hatua za kuhakikisha wanaweka njia za kuzuia lugha za asili kupotea.

Pia ameshauri shule kuchangia kwa kiasi kikubwa katika utunmzaji wa lugha za asili kwa kuziingiza katika mitaala huku jamii ya asili mayo ikiona kuwa utunzaji wa lugha za asili ni utunzaji wa historia zao na vile vile ndimo maono ya kisayansi yanamwotunzwa, busara, na shughuli za jamii zinazosogeza jamii kutoka hatua moja kwenda nyingine.