Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa dunia unaohusu wakimbizi waanza Geneva baada ya muongo mmoja wa kuhama

Wahamiaji na wakimbizi kutoka nchi tofauti wakiwasili kwa treni maalumu katika mji wa Berlin Ujerumani
UNICEF/Ashley Gilbertson VII
Wahamiaji na wakimbizi kutoka nchi tofauti wakiwasili kwa treni maalumu katika mji wa Berlin Ujerumani

Mkutano wa dunia unaohusu wakimbizi waanza Geneva baada ya muongo mmoja wa kuhama

Wahamiaji na Wakimbizi

Mkutano wa siku tatu wa dunia nzima wenye lengo la kubadilisha jinsi dunia inavyoshughulikia masuala ya wakimbizi unaanza leo mjini Geneva, Uswisi.

Mkutano huo wa kwanza wa aina yake unawaleta pamoja wakimbizi, wakuu wa nchi na serikali, viongozi wa Umoja wa Mataifa, mashirika ya kimataifa, mashirika ya maendeleo, wafanyabiashara na wawakilishi wa mashirika ya umma, miongoni mwa wenginie katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva.

UNHRC inaandaa mkutano huo kwa pamoja na Uswisi, mkutano ambao pia umeitishwa na Costa Rica, Ethiopia, Ujerumani, Pakistan na Uturuki.

Lengo la mkutano huu ni kutoa mielekeo mipya na mikakati ya muda mrefu kuwasaidia wakimbizi na jamii ambapo wao huishi.

Kote duniani zaidi ya watu milioni 70 wamehama kutokana na vita, mizozo na mateso.

Zaidi watu milioni 25 kati yao ni wakimbizi, wakiwa wamevuka mipaka ya kimataifa na hawana uwezo wa kurudi makwao.

Kamishina Mkuu wa UNHCR Filippo Grandi amesema, "tuko katika kipindi ambacho idadi ya wakimbizi imeongezeka, wiki hii kwenye mkutano wa kwanza wa dunia kuhusu wakimbizi, ni lazima tuweke jitihada zetu katika miaka inayokuja kwa kuwasaidia wakimbizi na nchi pamoja na nchi zinazowahifadhi."

Mkutano huu pia utajadili jinsi shughuli za kibinadamu na za kimaendeleo zinaweza kujumuika. Pia ni ishara ya kuongezeka umuhimu wa wajibu wa sekta za binafsi ambapo zaidi ya kampuni 100 na wakfu zinahudhuria, na zinatarajiwa kutoa ahadi za ajira,  fedha na misaada mingine.