Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ugiriki mmejitahidi lakini acheni kuweka watu vizuizini:UN

Wakimbizi na watoto wahamiaji waishio katika kituo cha mapokezi Moria, sehemu za Lesvos, Ugiriki
UNICEF/Pavlos Avagianos
Wakimbizi na watoto wahamiaji waishio katika kituo cha mapokezi Moria, sehemu za Lesvos, Ugiriki

Ugiriki mmejitahidi lakini acheni kuweka watu vizuizini:UN

Haki za binadamu

Wataalam wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifai wameipongeza serikli ya Ugiriki kwa hatua kubwa katika mchakato wa kukomesha kuweka watu kizuizini lakini bado ina changamoto kubwa kutokana na kusambaa kwa  vitendo vya kusweka watu vizuizini katika mfumo wa haki na uhalifu na mifumo ya uhamiaji ambayo lazima imalizike.

Wakihitimisha ziara yao ya siku 10 nchini humo wataalam hao wa haki za binadamu wamesema "Tunatambua na kusifu juhudi za Ugiriki za kushughulikia masuala ya kukomesha kuweka watu kizuizini kwa njia ya sheria mbadala, vifungu vya watu kutolewa mapema na mipango ya kuwaachilia kutoka kwenye vizuizi watu wenye ulemavu.”

Wataalam hao wamesema ushirikiano uliotolewa na serikali na nia yake ya kuwezesha fursa za kufika katika maeneo yote ya vizuizi, kule kulikotangazwa na ambako hawakutangaza ulikuwa mzuri sana na wamesema huo uwe mfano wa jinsi ya kushirikiana na makundi ya haki za binadamu yanapofanya ziara katika nchi zingine.

Hata hivyo wataalam hao wamesema , “utumiaji wa vizuizi bado unaendelea katika mfumo wa haki ya makosa ya jinai na uhamiaji na tunahimiza Ugiriki kumaliza sera hii. Inatia wasiwasi kuwa imekuwa ni hatua ya kawaida, licha ya matakwa ya sheria ya kimataifa kwamba inapaswa kutumika tu kama hatua ya mwisho. Matumizi ya sheriaya kuweka watu vizuizini kabla ya kesi inapaswa kutumiaka tu kwa nadra na sio utaratibu wa kawaida”

Wataalam hao wamependekeza kwamba utekelezaji wa njia mbadala wa kizuizini utasaidia pia kupunguza msongamano katika jela na mahabusu. Wataalam hao wamesema Ugiriki inaendelea kukabiliwa na changamoto kubwa katika suala la uhamiaji  hasa ikizingatiwa mahali ilipo kusini mwa mpaka wa Muungano wa Ulaya.

“Ni muhimu sana kwamba mtazamo wa kikanda ukachukuliwa ili kushughulikia suala lauhamiaji kwa kuheshimu haki za binadamu za wahamiaji wote ikiwemo wanaosaka ulinzi wa kimatyaifa. Kuwaweka kizuizini wahamiaji inapaswa tu kuwa ni kama suluhu ya mwisho kwa kuzingatia tathimini ya kila muhamiaji na iwe kwa kipindi kifupi.”

Wataalam hao wamesema pia mabadiliko ya sheria ya hivi karibuni ambayo itaanza kutumika rasnmi mwezi Januari 2020 yanatia hofu hususan kuongeza kwa muda wa mwisho wa kuweka watu kizuizini.

“Hii haiendani na wajibu wa kimataifa wa haki za binadamu unaopaswa kutekelezwa na Ugiriki. Na pia tuna wasiwasi mkubwa kwamba watoto wanaosafiri peke yao  na watoto wengine wanashikiliwa na kuchukuliwa kama watu wazima kuweka watoto mahabusu kwa minajili ya uhamiaji kunapigwa marufuku chini ya sheria za kimataifa na lazima kukomeshwe.”

Kundi hilo la wataalam limeitaka serikali kuchapuza mchakato wa kuwatoa kizuizini watu wenye ulemavu kwa mujibu wa mkataba wa kimataifa ambao Ugiriki imeridhia.

Wakati wa ziara hiyo ya siku 10  tangu Desemba 2 hadi Desemba 13 mwaka huu wataalamu hao , Jose Antonio Guevara Bermúdez, Leigh Toomey na  Sètondji Roland Adjovi, walikutana na maafisa wa serikali, majaji, wanasheria, mawakili, wawakilishi wa asasi za kiraia na watu wengine muhimu.  

Walifanikiwa kutembelea vituo 20 vya mahabusu na kuwahoji zaidi ya watu 150 ambao wananyimwa uhuru wao.

Ripoti ya mwisho kuhusu ziara yao itawasilishwa kwenye Baraza la Haki za binadamu mwezi Septemba 2020.