Wakimbizi 183 waliokuwa Chad wapata makazi mapya Ufaransa:IOM

13 Disemba 2019

Wakimbizi 183 waliotokea Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR na kusaka hifadhi nchini Chad , leo wamewasili Ufaransa kwa ajili ya makazi mapya kupitia mpango wa shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM.

Kwa mujibu wa IOM ndege hiyo iliyowasili leo ndio inafunga pazia la operesheni ya miaka miwili ya IOM ambayo imesaidia kuwapa makazi mapya zaidi ya wakimbizi 1700 kutoka Chad kwenda kwenye nchi za Muungano wa Ulaya.

Wakimbizi hao wamekuwa wakiishi kwenye makambi ya wakimbizi mashariki mwa Chad na majimbo mengine ya kusini lakini pia N’Djamena mji mkuu wa nchi hiyo.

Wakimbizi kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, Nigeria na Sudan Kusini wamekuwa wakiishi katika kambi za wakimbizi.

Mmoja wa wakimbizi hao Said Abakar baada ya kuwasili amesema “tulikimbia nchi yetu kwa sababu ya vita na tulikuja Chad kusaka usalama. Na sasa tuko Ufaransa tutakuwa na utulivu zaidi na maisha mapya.”

Mbali ya kutoa usafiri huo wa ndege , IOM nchini Chad imekuwa ikiwapa wakimbizi taarifa na mafunzo kabla ya kuondoka , kuwafanyia uchunguzi wa afya na kuwapa huduma kama wanahitaji na pia msaada wa kiufundi na kuchagua baadhi yao ambao watafanyiwa usaili na mamlaka ya Ufaransa na Chad.

Baada ya kuwasili wakimbizi hao wamepokelewa na mashirika ya Ufaransa yasiyo ya kiserikali NGO’s ambao mara moja waliwapa msada wa haraka uliohitajika. NGO hizo pia zitawasaidia katikamakazi mapya nchini Ufaransa kwa mwaka wote wa kwanza hasa katika masuala ya makazi, kusoma kozi za lugha ya Kifaransa na kuwapa nyenzo za kuwasaidia kujumuika katika jamii mpya.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter