Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kampuni ya Volkswagen yaonyesha kwa vitendo maana ya utangamano na wakimbizi

Wahamiaji wakisubiri kusajiliwa mjini Berlin, Ujerumani
Picha ya UNICEF/UNI199995/Gilbertson V
Wahamiaji wakisubiri kusajiliwa mjini Berlin, Ujerumani

Kampuni ya Volkswagen yaonyesha kwa vitendo maana ya utangamano na wakimbizi

Wahamiaji na Wakimbizi

Nchini Ujerumani mafunzo mahsusi yanayotolewa na kampuni za kijerumani kwa wakimbizi yameleta siyo tu matumaini kwa wakimbizi bali pia kusaidia kujenga utangamano na jamii zinazowazunguka.

Hapa ni mjini Baunatal nchini Ujerumani, mkimbizi kutoka Afghanistan Mastura Ekhlas ambaye pia ni mama watoto watatu akiwa kazini kwenye bohari ya kampuni ya kutengeneza magari ya Volkswagen.

Uwezo wa kuendesha foko hii unafuatia mafunzo yanayotolewa na mtandao wa kampuni za kijerumani kwa ajili ya wakimbizi.

Kwa kuongeza mafunzo ya lugha ya kijerumani na za kazi, waajiri wanasaidia wageni kukabiliana na changamoto mpya za mazingira mapya ya kazi.

Katika bohari hii ya Volkswagen, wakimbizi wanakuwa na miaka miwili ya kujifunza kazini na programu pia ya kuwawezesha kuingia katika soko la ajira la Ujerumani.

Programu hii ilizinduliwa mwaka 2017, na inatekelezwa kwenye kiwanda cha pili cha ukubwa cha Volkswagen hapa Baunatal kwa kuwa wanataka kukidhi mahitaij ya usafirishaji na usambazaji wa bidhaa.

Wahitimu wanaajiriwa kama siyo na Volkswagen basi na kampuni nyingine kwenye eneo hili.

Mastura ameweza kukabili changamoto za mazingira mapya ya kazi na anasema, "kufanya kazi  hapa VW katika mwaka wa kwanza haikuwa rahisi. Nilifanya kazi mwaka mzima kwa bidi zote. Kwa kuwa niko Ujerumani, nimekuwa na mtazamo chanya. Mwanzoni kulikuwa na shida kubwa. Lakini nalazimika kujipanga pia maisha yangu binafsi, si jambo rahisi.”

Mnufaika mwingine ni Mohammad Al Jaser, mkimbizi kutoka Syria na anasema, "hii ni muhimu pia kwa familia yangu. Wanajivunia sana. Sifanyi kazi kwa ajili yangu tu, bali pia kwa familia yangu, wazazi wangu na mwanangu.”

Dkt. Stefan Kreher ni Mkurugenzi wa rasilimali watu, katika ofisi  ya Volkswagen Baunatal na anafunguka ya kwamba, "nafikiri kuwa na ajira kuna nafasi muhimu sana katika kufanikisha utangamano. Hii inaweza kumaanisha kazi yenye stadi kamili, lakini muhimu zaidi kazi inayopatia watu matumaini.”

Kampuni ya Volkswagen imekuwa ikisaidia wakimbizi tangu wimbi la kuwasili la mwaka 2015 ambapo awali iliangazia katika misaada ya dharura na hatimaye kampuni hiyo ikaamua kuwapatia wakimbizi misaada ya kimkakati ikiwemo ajira za muda mrefu.

TAGS: UNHCR, Volkswagen, Baunatal