Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukosefu wa usalama ukichochea visa vya Ebola, DRC, sasa watoa chanjo kutumia helkopta- WHO

Wafanyakazi wa kituo cha Ebola cha Katwa Butembo, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC wakisafisha viatu na nguo
UN Photo/Martine Perret
Wafanyakazi wa kituo cha Ebola cha Katwa Butembo, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC wakisafisha viatu na nguo

Ukosefu wa usalama ukichochea visa vya Ebola, DRC, sasa watoa chanjo kutumia helkopta- WHO

Afya

Shirika la afya ulimwenguni WHO limesema visa vipya vya Ebola 27 vilivyothibitishwa vimeripotiwa katika majimbo ya Ituri na Kivu kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC. 


WHO inasema visa hivyo vimethibitishwa juma hili katika vituo saba vya afya vilivyo katika kanda nne zinazotibu Ebola ambapo Mabalako kumekuwa na visa 18, Beni 6, Mandima visa 2 na Oicha kisa kimoja.

Shirika hilo limeongeza kuwa hii ni idadi kubwa ya visa vipya vinavyoripoitiwa ukilinganisha na visa saba vilivyothibitishwa katika wiki tatu zilizopita.

Dkt Michel Yao ambaye ni meneja wa ufuatiliaji wa Ebola nchini DRC amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva, USwisi hii leo kuwa sababu kuu ya ongezeko hilo la ghafla ni ukosefu wa usalama kwa kuwa awali ilikuwa ni chini ya visa 10 kwa wiki lakini sasa 27 na kutokana na ukosefu wa  usalama..

Amesema kwamba, ukosefu wa usalama, "unatuzuia kufikia jamii kuwakinga dhidi ya Ebola. Na wakati huo huo wananchi wanakabiliwa na mauaji yanayotokana na ghasia ambazo pia zimezuia hatua za kukabiliana na Ebola. Hatuwezi  kufanya kazi ya  ufuatiliaji ikiwemo chanjo ambayo imekuwa moja  ya mbinu bunifu iliyosaidia kuzuia kuenea kwa mlipuko nchini humo. "

Dkt. Michel Yao,Mtaalamu WHO
WHO
Dkt. Michel Yao,Mtaalamu WHO

Watoa chanjo sasa kutumia helikopta 

Kutokana na  changamoto za usalama, WHO sasa imeamua kuwa watoa chanjo watakuwa wanatumia helikopta ili kufikia jamii zilizo kwenye maeneo yenye mapigano. Timu ya kwanza ya kutoa chanjo kwa kutumia helikopta ilifanya hivyo jana Alhamisi ambapo Dkt. Yao amesema, “helikopta hiyo tunayotumia ina nafasi ya watoa huduma 20 hii ikimaanisha kuwa tunaweza kusafirisha wafuatiliaji wa Ebola lakini pia watoa chanjo."

Yasadikiwa kuwa kuna vikundi  tarkibani 100  vilivyojihami ambavyo vinashambulia kwenye eneo la  mashariki mwa DRC mpakani na Uganda, Rwanda na Burundi na hivyo kusababisha janga la kibinadamu kwa wakazi wa maeneo hayo.

Mgonjwa mmoja kaambukiza wagonjwa 17

Visa vyote vya sasa vinahusiana na mnyororo wa maambukizi matatu.Na kati ya visa hivyo 27 visa 20 vimeelezwa ni kutokana na kukutana na mgonjwa na  10 kati ya hivyo vilikuwa vikifuatiliwa.

Ni kisa kimoja ya mtu kufa ndicho kimeripotiwa  wakati akisafirishwa kutoka kituo cha afya cha Lwemba ili kuepusha maambukizi na mtu huyo alizikwa kwa utaratibu na heshma zote.

Na visa vingine vyote vilipelekwa kwenye vituo vya afya vya kutibu Ebola.

Lakini WHO inasema visa vyote hivi vinahusishwa na mnyororo wa mtu mmoja ambaye anaonekana kuwa chanzo cha watu 17 kupata maambukizi. Na hii ni mara ya pili mtu huyo kuripotiwa mgonjwa katika kipindi cha mizei sita.

Hadi kufikia tarehe 10 mwezi huu wa Desemba 10 jumla ya visa 3340 vya Ebola vimeripotiwa  vikiwemo visa 3222 vilivyothibitishwa, visa 118 vinavyoshukiwa na watu 2210 waliopoteza maisha.