Mwaka 2020 kuwa 'mwiba' kwa watu milioni 5.5 nchini Sudan Kusini

12 Disemba 2019

Shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa WFP limesema linakimbizana na muda ili kukusanya fedha zinazohitajika kuwalisha mamilioni ya watu Sudan Kusini wakati huu njaa ikishika kasi na watu wanaohitaji haraka msaada wa kibinadamu.

 Shirika hilo limelaumu ukame, sintofahamu ya mustakbali wa kisiasa na mafuriko makubwa yaliyotokea katika miezi ya karibuni kuwa vimelipeleka taifa hilo na watu wake katikahali mbaya mwaka ukikaribia ukingoni.

Takriban watu milioni 5.5 wanatarajiwa kukabiliwa na njaa mapema mwaka 2020 limesema shirika hilo huku idadi ya watu watakaohitaji msaada wa kibinadamu ikitarajiwa kuongezeka  kwasababu ya uharibifu mkubwa uliosababishwa na mafuriko tangu mwezi Oktoba baada ya ukame ambao uliathiri sehemu kubwa ya nchi na kuharibu mazao.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa WFP David Beasley “Kwa majanga yote tunayoyashuhudia duniani kitu cha mwisho tunachokihitaji ni ni kutotokea kwa janga lingine, tunayajua matatizo ambayotumekuwa nayo Sudan Kusini , lakini mvua na mafuriko vimesababisha janga la kitaifa na kubwa na baya kuliko kila mtu alivyotarajia. Na endapo tusipopata fedha za ufadhili katika wiki au miezi michache ijayo tutakuwa tunazungumzia baa la njaa, tunahitaji msaada na tunauhitaji sasa.”

Takribani watu milioni moja wameathiriwa moja kwa moja na mafuriko ambayo yamesambaratisha tani 73,000 za uwezekano wa mavuno na kuangamiza maelfu ya ng’ombe na mbuzi ambao wanategemewa na watu wengi kwa ajili ya kuishi.

Msaada wa kibinadamu unaokoa maisha katika maeneo mengi Sudan Kusini. Mwaka 2019 WFP ilijitahidi kuwafikia watu milioni 4.6 na msaada wa kuokoa maisha lakini sasa inahitaji dola milioni 270 kwa ajili ya nusu ya kwanza ya mwaka 2020 na kwa mwezo ujao WFP inahitaji dola milioni 100 kwa ajili ya kununua chakula kabla ya msimu wa mvua kuanza Mei 2020.

Mwezi Oktoba mwaka huu serikali ya Sudan Kusini ilitangaza hali ya dharura katika majimbo ya Bahr El Ghazal, Greater Upper Nile na Greater Equatoria kwa sababu ya mafuriko na kuomba kuongezwa kwa msaada wa kimataifa.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud