Mradi wa maji wa kutumia nishati ya jua au sola waleta neema kwa wakimbizi Uganda

11 Disemba 2019

Mradi wa maji safi na salama unaoendeshwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi kwenye makazi ya wakimbizi ya Bidibidi nchini Uganda umekuwa faraja sio tu kwa wakimbizi bali pia jamii zinazowahifadhi. 

Miongoni mwa wakimbizi hao ni  Asharose Sillah aliyefungasha virago na kukimbia vita Sudan Kusini mwaka 2016.  Hivi sasa Asharose anaishi  katika makazi ya wakimbizi ya Bidibidi nchini Uganda .

Asharose anasema kuwa, "tulipoletwa hapa ilikuwa ni msimu wa mvua , malori yalikuwa yamekwama barabarani na ilikuwa vigumu sana kwetu kupata maji . Sisi kama wanawake tulikuwa tunang’ang’ana wote kupata maji kwenye gari hilohilo lililokuwa likileta na idadi ya watu ilikuwa kubwa sana.”

Asharose alipowasili Uganda kwa mara ya kwanza wakimbizi iliwabidi kupanga foleni kwa saa kadhaa na maji yalikuwa yakiletwa na malori kutoka mbali kama kilometa 100 hivi. 

Lakini sasa kituo cha maji kipo kilometa chache tu kutoka nyumbani kwake na anasema kuwa, “hivi sasa kila Kijiji kina angalau mabomba 3 hadi 4 na ukiangalia ukaona kuna watu wawili hapo unaenda ambako kuna mtu mmoja na ukienda inakuokolea muda kila wakati unapoenda kuchota maji"

Mradi huu wa maji wa shirika la kuhudumia wakimbizi UNHCR unaoendeshwa kwa nishati ya jua au sola unaleta mabadiliko makubwa ukiwa na uwezo wa kutoa lita 85,000 kwa saa na kuwanufaisha wakimbizi 200,000 wa kambi ya Bidibidi na jamii zinazowahifadhi.

Awali maisha ya wakimbizi na jamii yalikuwa magumu kwani walikwenda mwendo mrefu kusaka maji na iliwabidi kuchimba visima  na sasa wanasema asante UNHCR, yaliyopita si ndwele wanaganga yajayo.

TAGS:UNHCR, Bidibidi, Uganda, wakimbizi, Sudan Kusini, maji

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter