Milima ni muhimu kwa vijana na mustakabali wetu:FAO

Nchini Nepal na ni taswira ya mji mkuu Kathmandu na kwenye miteremko ya milima ni makazi ya watu na vyanzo vya vipato pamoja na mashamba ya mazao ya chakula
UN Photo/Gill Fickling
Nchini Nepal na ni taswira ya mji mkuu Kathmandu na kwenye miteremko ya milima ni makazi ya watu na vyanzo vya vipato pamoja na mashamba ya mazao ya chakula

Milima ni muhimu kwa vijana na mustakabali wetu:FAO

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya milima vijana wameelewa kuwa ndio wanaoendesha ajenda ya mabadiliko ya tabianchi na wanaweza kusaidia katika nyanja zote ikiwemo mfumo wa maisha kupitia milima.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO katika ujumbe wake wa kuadhimisha siku ya kimataifa ya milima hii leo, ujumbe ambao ametoa huko Madrid, Hispani kwenye mkutano wa 25 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko  ya tabianchi, COP25.

Qu Dingyu amesema “vijana wana jukumu kubwa la kufanya katika kudai msaada kwa ajili mfumo wa Maisha ambao uko matatani kutokana na njaa na hatari za mabadiliko ya taibianchi, kwani milima ni muhimu kwa vijana na kwa mustakabali wetu.”

Ameongeza kuwa “siku hizi kila mara tunaangalia mbele tu lakini tunasahau kuangalia tulikotoka, mfumo wa Maisha wa milima yet una faida zake kwa sayari hii viko katika tishio kubwa”.

Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya jopo la wataalam kuhusu mabadiliko ya tabianchi IPCC , mabadiliko hayo yanachochea theluji kuyeyuka huku ukataji miti, mmomonyoko wa ardho, uchimbaji madini na kilimo kisichoendelevu vyote pia ni tishio kubwa.

Kauli mbiu yam waka huu “milima ni muhimu kwa vijana” na  inatokana na ukweli kwamba milima inachukua takribani asilimia 27 ya uso wa dunia na ni makazi ya watu bilioni 1.1.

FAO inasema mwaka 2017 watu milioni 346 walikuwa katika hatari ya kutokuwa na uhakika wa chakula katika maeneo ya vijijini milimani hususani kwenye nchi zinazoendelea ikiwa ni ongezeko la asilimia 12 kimataifa tangu mwaka 2012 na ongezeko ni takriban mara mbili barani Afrika.

Milima pia inachangia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa maji na ni maeneo ambako mazao mengi hustawi kama mahindi, viazi mbatata, mtama, nyanya , shayiri na matufani mazao sita kati ya 20 abayo leo hii yanachangia asilimia 80 ya chakula duniani.

Kuhusu mchango wa vijana katika masuala ya milima FAO inasema ushirikishwaji wa vijana umedhihirisha kuzaa matunda kama ilivyoonyesha kwenye shughuli mbalimbali za ushirika wa milima kwa mfano ushirika huo umesaidia kuchagiza umuhimu wa maharage ya jumla , aina ya maharage yaliyopewa jina la mji wa wilaya moja huko Nepal ambayo yanasaidia kuinua kipato cha jamii na kuwawezesha vijana na wanawake katika kilimo cha familia kuweza kusomesha watoto wao.